Hamisa Mobetto ajibu wimbo wa Harmonize akimtaka kuwa mpango wake wa kando

Katika wimbo huo uliozua mtanziko mitandaoni, Harmonize alisikika akilia kwa huruma na kumtaka Hamisa Mobetto kumkubalia ili yeye [Harmonize] awe kama mpango wake wa kando japo kidogo tu.

Muhtasari

• Hamisa alikiri kwamba wimbo huo ameusikia lakini akasema hana lolote la kuweza kujibu zaidi ya hapo.

• Hata hivyo, mrembo huyo alisisitiza kwamba yeye ni mke wa mtu na hivyo mwanamume yeyote anayemmezea mate akae akijua hayupo sokoni tena.

Harmonize na Hmisa Mobetto.
Harmonize na Hmisa Mobetto.
Image: Insta

Msanii ambaye pia ni mjasiriamali Hamisa Mobetto hatimaye amevunja kimya chake siku chache baada ya Harmonize kuachia wimbo akimuimbia mwanamke ambaye alikisiwa kuwa Hamisa Mobetto akimtaka kuwa kama mpango wake wa kando.

Wikendi iliyopita Harmonize alitanagaza kuachia EP yenye ngoma 7 ambapo aliirekodi ndani ya saa 24 na katika kionjo cha wimbo mmoja, alimuimbia mwanamke kwa kutoa maelezo yaliyoashiria moja kwa moja ni Hamisa aliyekuwa akiimbiwa.

Harmonize alikuwa anamtaka Hamisa Mobetto kumchukua kama mchepuko wake, kipande cha wimbo ambacho kimezua minong’ono mingi mitandaoni ikizingatiwa kwamba mrembo huyo amewahi toka kimapenzi na Diamond ambaye ni hasidi wa Harmonize.

Hamisa katika live kwenye Instagram yake alizungumzia suala hilo na kusema kwamba hata yeye ameisikia mitandaoni kama mtu mwingine yeyote, huku akisisitiza kwamba yeye ni mke wa mtu kwa hiyo haiwezekani kulikubali ombi la Harmonize.

“Naona kuna watu wengi sana wanauliza kuhusu masuala ya sijui nyimbo, sijui kutungiwa wimbo. Nyimbo niliisikia kama nyinyi mlivyoisikia ndugu zanguni na mimi mwenyewe niliisikia huku Insta kama nyinyi mlibyoisikia. Kwa hiyo sina cha kuelezea kwa sababu hata mimi nipo tu kama nyinyi. Hata sikujua kama inanihusu kwa hiyo hata mpaka lepo hii hata mimi nimeiona hivyo hivyo na nikaiacha hivyo hivyo,” Hamisa alisema.

“Kwa hiyo sina cha kujibu lakini kumbukeni jamani mimi ni mke wa mtu, shemeji yenu yaani anaupiga mwingi,” Hamisa aliongeza.

"Sijui kama ni wakati mwafaka wa kusema hivi. Ninachojua ni kwamba sina budi kukuambia hili. Umbo lako la mwili linanifanya nifanye hivi. Je, unaona? Mpenzi natumai unajua hili. Najua una mwanaume. Unaonekana unaenda kuwa mke wa mtu. Naweza kuwa mtu wako bora. Usinipoteze, nifanye tu mpango wako wa kando,” Konde Boy aliimba katika wimbo huo ambao aliachia mwishoni mwa wiki iliyopita.

 Anaendelea, "Je, huoni sura yako nzuri kwenye wallpaper yangu? Hiyo ina maana niko tayari kukupa karatasi yangu yote (Baby karatasi yangu yote). Acha niwe mpango wako wa kando (x5). Nataka kuwa mpango wako wa kando. Mpenzi nifanye kuwa mpango wako wa kando. Naapa nasubiri hadi uwe wangu."