Ananipa nguvu zaidi-Rashid Abdalla afunguka kuhusu kufanya kazi na mkewe Lulu Hassan

“Kasiri ambako watu hawakajui ni kwamba mimi napenda kazi yangu lakini niliye naye karibu yangu ananipa nguvu zaidi

Muhtasari
  • Kwa mujibu wake, Lulu si mrembo tu ambaye alimuoa bali pia ni rafiki yake mkubwa na ndiyo maana wanaratibu vizuri sana wakiwa wanafanya kazi pamoja na nyumbani kwao.
Rashid Abdalla amtakia kheir ya kuzaliwa mkewe Lulu Hassan.
Rashid Abdalla amtakia kheir ya kuzaliwa mkewe Lulu Hassan.
Image: INSTAGRAM// RASHID ABDALLA

Mtangazaji mashuhuri wa Habari za Kiswahili Rashid Abdalla amefunguka kuhusu kufanya kazi na mkewe Lulu Hassan.

Wawili hao huandaa habari za wikendi katika runinga ya Citizen na wanaendesha kampuni ya kutengeneza filamu inayojulikana kama Jiffy Pictures.

Akizungumza katika mahojiano na Mpasho, Rashid alisema kuwa Lulu ndiye msukumo wake mkubwa kutokana na mapenzi aliyonayo kwenye miradi yao.

“Kasiri ambako watu hawakajui ni kwamba mimi napenda kazi yangu lakini niliye naye karibu yangu ananipa nguvu zaidi namzungumzia mke wangu Lulu Hassan ana mapenzi ya dhati kwa kazi tunayoifanya ana mapenzi ya dhati kuweza kusaidia vijana sisi wenyewe ni vijana. Hakuna mwigizaji mbaya, ni kama hajapewa fursa, lakini cha msingi ni ijapo fursa zile sifa zikafanya akabweteka. Akasahau kuwajibitikia kazi yake. Sifa ni changamoto ufanye utie bidii,” alieleza.

Kwa mujibu wake, Lulu si mrembo tu ambaye alimuoa bali pia ni rafiki yake mkubwa na ndiyo maana wanaratibu vizuri sana wakiwa wanafanya kazi pamoja na nyumbani kwao.

“Kusema ukweli mimi sikuoa mrembo nimeoa rafiki yangu, kwa hivyo mimi sina wasi kuwa na rafiki yangu nje ya nyumba na ndani ya studio. Ukifanya kazi na mtu ambaye ni rafiki yako hakuna fegisu fegisu ..unatoboa tu maana mimi nafurahi tu niko na rafiki yangu. Rafiki ambaye ukikosea atakuambia ukweli , rafiki hakufichi labda rafiki wa uongo na rafiki analilia kukukosoa,” mwandishi wa habari wa Citizen TV alisema.

Wakati huo huo alifichua siri nyuma ya mafanikio yake.

“Kuomba na kujituma. Siri ni kuomba. Kwanza nashukuru yale kampuni yana tuamini kama vile Maisha Magic twashukuru, anayetengeneza stori mzuri, siri kuwa na watu wazuri, kwanzia mpishi mpaka kuendesha gari,” alisema.

"Ni ushirikiano, kama hakuna kudumu hakuna kwenda mahali," Rashid aliendelea kusema.