"Ndoa ni ngumu tena ni tamu" Simon Kabu asema akishauri kuhusu ndoa

"Kwa hiyo mnafaa kuwa waelewa, usiingie kwa ndoa ukifikiria mwenzako hatakosea, atakosea. Lakini akikosea huwa unalimudu aje? " Kabu alisema.

Muhtasari

• Kabu alisema kwamba watu wengi huanza kupata changamoto haswa wanapobarikiwa na Mungu haswa kwa upande wa mali.

• Mjasiriamali huyo alishauri kwamba katika ndoa, shina kubwa ni mazungumzo wala hakuna kitu kingine.

Simon Kabu.
Simon Kabu.
Image: Screengrab

Mjasiriamali wa kampuni ya utalii ya Bonfire Adventures Simon Kabu ametoa ushauri kuhusu ndoa, akiwa kama mmoja wa watu maarufu ambao wamedumu kwa ndoa kwa miaka mingi.

Akizungumza na SPM Buzz, haswa baada ya Kate Actress na mumewe Phil Karanja ambao walikuwa marafiki wake wa karibu kutengana, Kabu alishauri kwamba yeye na mkewe Sarah Kabu licha ya kwamba wamedumu pamoja kwa muda mrefu haimaanishi kwamba hapajawahi tokea mfarakano.

Kabu alikiri kwamba mambo ya ndoa ni magumu sana lakini pia akasema wakati wanandoa wanaelewana, ndoa inaweza ikawa tamu kuliko kitu kingine chochote.

“Kwanza mambo ya ndoa ni magumu, unasikia watu wanasema watu wawili waliojifunika blanketi mmoja usiongee chochote kuwahusu. Sasa kuna upande wa hisia katika hilo lakini ukweli ni kwamba ndoa ni tamu,” alisema.

“Ninasema hivyo kwa sababu mimi na mke wangu Sarah tunafanya kazi pamoja na tunatembea na yeye kila sehemu kila sehemu huwa na tunakaa pamoja. Kwa hiyo mnafaa kuwa waelewa, usiingie kwa ndoa ukifikiria mwenzako hatakosea, atakosea. Lakini akikosea huwa unalimudu aje? Wanasema watu wanaocheza pamoja hukaa pamoja lakini siku hizi tunasema watu wanaosafiri pamoja hukaa pamoja,” Kabu aliongeza kwa furaha.

Kabu alisema kwamba watu wengi huanza kupata changamoto haswa wanapobarikiwa na Mungu haswa kwa upande wa mali.

Mjasiriamali huyo alishauri kwamba katika ndoa, shina kubwa ni mazungumzo wala hakuna kitu kingine.

“Mazungumzo ndio kitu cha muhimu Zaidi katika ndoa hakuna kitu kingine. Kuelewana na kusoma mwenzako, unamsamehe na mnaongea, na wewe ukisamehewa usirudie makosa. Vitu vingi ambavyo watu wanakosana navyo ni hivi vidogo vidogo, si mambo makubwa. Lakini mkielewana inakuwa sawa,” alisema.