Nafikiria kuachana na maisha ya mjini nirudi shambani kwa ukulima - Charlene Ruto

“Ni jambo la kuridhisha sana, nikifanya huwa naona matokeo ya kile ambacho nakifanya na ni kitu cha kukutuliza na kuna amani. Hakuna mambo mengi, hakuna msongamano wa magari, hakuna kusuguana na watu sana."

Muhtasari

• Charlene alifichua kwamba amefanya ukulima kwa mwaka mmoja hivi akisema kwamba mwaka jana ndio alianza kuchukulia ukulima kwa uzito.

Charlene Ruto
Charlene Ruto
Image: Twitter

Binti wa kwanza wa taifa Charlene Ruto amefunguka kwamba anawazia kuachana na maisha ya mjini na kurudi mashambani.

Katika mahojiano na SPM Buzz, bintiye Ruto alisema kwamab licha ya kwamba anajihusisha sana katika masuala mbali mbali yakiwemo jkujifunza lugha ya ishara kuwasiliana na viziwi, lakini pia anajitahidi kufanikisha kazi yake shambani.

Alisema kwamba kwa sasa anajaribu kusawazisha kati ya mitikasi ya mjini na shambani lakini kwa asilimia kubwa roho yake inaegemea sana shambani.

“Kusema ukweli ukulima nauchukulia kwa uzito sana, huwa naenda shambani mara kwa mara kadri ya uwezo wangu. Kwa sasa najaribu kusawazisha kuwa mjini na kwenda shambani lakini nafikiria pengine nihamie shambani kabisa. Kusema ukweli nawazia sana kuchukua mkondo huo,” Binti Ruto alisema.

Charlene alitetea wazo hilo akisema;

“Ni jambo la kuridhisha sana, nikifanya huwa naona matokeo ya kile ambacho nakifanya na ni kitu cha kukutuliza na kuna amani. Hakuna mambo mengi, hakuna msongamano wa magari, hakuna kusuguana na watu sana, ni maisha ya Amani sana. Pia nikiwa shambani huwa Napata kufikiria na kufungua mawazo.”

Charlene alifichua kwamba amefanya ukulima kwa mwaka mmoja hivi akisema kwamba mwaka jana ndio alianza kuchukulia ukulima kwa uzito.

“Nimefanya ukulima wa kiwango cha juu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Ukulima mkubwa kwangu kwa sasa hivi ni kufuga nyuki. Bado naendelea kujifunza kama huwa naenda shambani kuchukua mimea mbalimbali iliyopo na nina watu wengi vijana ambao wananisaidia kufanya hivyo. Lakini kwa sasa ukulima mkuu kwangu ni ufugaji wa nyuki,” alisema.

Binti huyo ambaye amefuata nyayo za babake katika ukulima alitangaza kwamab mwishoni mwa mwezi Septemba atazindua mpangilio maalum wake ambao utatoa mwanga kwa vijana wengine kufuata.