Bahati amenitoa mbali sana, penye niko sasa hivi ni kwa sababu yake - Diana Marua

“Bahati hakuwahi kunitupia maneno ya kunitaka, ni mimi nilimwambia nataka kuwa rafiki yako. Wakati huo nilikuwa najua dhana ya jamii kwamba nisingeolewa kwa mwanamume mdogo kiumri kuniliko."

Muhtasari

• "Mimi nilichumbiana na wanaume wengi sana, wengi wao walikuwa na pesa. Bahati akinipata sikuwa nimekosa kitu,” aliongeza.

Diana Marua na Bahati.
Diana Marua na Bahati.
Image: Insta

Diana Marua kwa mara nyingine ameradidi kuhusu wajibu ambao mumewe Bahati ametekeleza katika maisha yake mpaka alipo sasa hivi kama mwanablogu namba moja wa YouTube.

Marua alifichua haya wakati wa kikao na wafanyikazi wake kweney sebule lake akisema kwamba siku zote ataishi kumheshimu Bahati kwa kutomfungia na badala yake kumpa uhuru wa kufanya kila kitu ambacho alikuwa anahisi angeweza kufanya bila vikwazo.

Marua alisema kwamba mpaka pahali amefikia sasa hivi kama mwanablogu namba moja, ni kutokana na juhudi za mumewe Bahati.

“Bahati mara nyingi anakuja na kuniambia kwamba watu wanamwambia kunisaidia kufanya kile nakipenda siku moja nitamuacha. Acha niwaambie ukweli, Bahati amenitoa mbali sana. Na mahali niko sasa hivi yote ni kwa sababu yake. Kila kitu ambacho Diana anafanya kutoka kukuza maudhui, kuwa mama yeye ndio amekuwa akinisukuma,” alisema.

Alikiri kwamba akikutana na Bahati alikuwa amechumbiana na wanaume wengine lakini hakuna hata mmoja kati yao ambaye anaweza kufikia viwango vile ambavyo Bahati alimfikisha.

“Nikikutana na Bahati, nilikuwa nimechumbiana huko nje na nimesema hili mara nyingi tu. Na wakati nilikuwa nachumbiana nilikuwa natafuta mapenzi ya kweli. Mimi nilichumbiana na wanaume wengi sana, wengi wao walikuwa na pesa. Bahati akinipata sikuwa nimekosa kitu,” aliongeza.

Muda wote huo Bahati alisema kwamba alikuwa anajua chenye anahitaji – hakutaka kuolewa ili kuwekwa ndani kama mwanamke, kitu ambacho wanaume wengine walikuwa wanamtakia.

Bahati alikuwa ni mtu mmoja ambaye alimchukua na kumpa maisha ambayo alikuwa anayatamani – maisha ya kupatiwa uhuru wa kufanya chenye angetaka kufanya.

Marua alifichua kwamba Bahati hakuwahi kumtupia maneno ya kumtongoza bali ni yeye mwenyewe alianza kwa kumwambia kwamba angependa kuwa rafiki yake.

“Bahati hakuwahi kunitupia maneno ya kunitaka, ni mimi nilimwambia nataka kuwa rafiki yako, sio kuwa mpenzi au mke wako. Wakati huo nilikuwa najua dhana ya jamii kwamba nisingeolewa kwa mwanamume mdogo kiumri kuniliko. Kwa hiyo nilitaka kuwa rafiki wa kweli kwa sababu alikuwa mtu tofauti,” alisema.

Baadae wakawa wanakutana na Bahati akawa anamhubiria na hapo ndipo mbegu ya mapenzi ilipoota.