Bahati, Diana wajivunia mtoto wao wa kulea, Morgan Bahati " ni moja ya baraka zetu kubwa!"

Wanandoa Bahati na Diana Marua wameendelea kudhirisha upendo wao mkubwa kwa mtoto wao wa kulea, Morgan Bahati.

Muhtasari

•Wameeleza kuwa mvulana huyo mwenye umri wa miaka 13 ni miongoni mwa baraka kubwa zaidi kutendeka katika maisha yao.

•Hivi majuzi akizungumza katika mahojiano na Chipukeezy, Bahati alimtaja mvulana huyo wa miaka 13 kama mtoto maalum.

Image: INSTAGRAM// BAHATI

Wanandoa maarufu Kelvin ‘Bahati’ Kioko na Diana Marua wameendelea kudhirisha upendo wao mkubwa kwa mtoto wao wa kulea, Morgan Bahati. 

Huku wanandoa hao mashuhuri wakikaribia kuadhimisha miaka saba ya ndoa yao, wameeleza kuwa mvulana huyo mwenye umri wa miaka 13 ni miongoni mwa baraka kubwa zaidi kutendeka katika maisha yao.

"Tunapokaribia kusherehekea kumbukumbu ya miaka 7 na ndoa yetu Oktoba hii, Morgan Bahati ni moja ya baraka zetu kubwa," Bahati alisema siku ya Jumapili kupitia Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha ya maktaba yake, mkewe Diana Marua na mwanawe huyo iliyopigwa miaka kadhaa iliyopita.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 alimchukua Morgan kuwa mtoto wake mwaka wa 2014 wakati alipoenda kutumbuiza katika nyumba ya  watoto yatima ya ABC ambapo alikulia pia baada ya mama yake kuaga dunia.

Baada ya Bahati kutumbuiza, mvulana huyo alikataa kurejea katika kituo hicho cha watoto na akataka kwenda naye.

Hivi majuzi akizungumza katika mahojiano na Chipukeezy, Bahati alimtaja mvulana huyo wa miaka 13 kama mtoto maalum.

Alifichua kwamba yeye humpa Morgan upendeleo sana hadi humlipia karo ya shule kabla hata hajawalipia watoto wake wengine.

"Kabla ata nilipie watoto wengine wangu karo huwa nalipia Morgan," Bahati alisema.

Aliongeza, “Huwa naishi naye. Unajua watu wengi mitandaoni wameanza kutufuatilia baada ya Diana. Huyu ni mtoto nimekuwa naye hata kabla niingie kwa ndoa. Kwa hakika, wanawake wengi walinikataa kwa sababu ya mtoto huyu kwa sababu hakuna ambaye alikuwa kukaa na mtoto si wake.”

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili pia alitumia fursa hiyo kuwasihi wanamitandao na wanablogu kuwa na utu wakati wa kuandika hadithi zinazomhusisha mwanawe huyo.

Alifichua kuwa Morgan ana kisa cha kuhuzunisha sana na hivyo kuwataka Wakenya kuepuka kumshambulia wakati wanapokuwa wakishambulia familia yake.

"Sina shida na mtu yeyote kushambulia familia yangu, watoto wangu. Lakini usiwe unamshambulia mtoto wangu wa kwanza, Morgan. Nilimchukua mvulana huyu wakati wa msimu mgumu sana wa maisha yangu. Huyu ni mtoto nilimtoa kwa children’s home.

“Ako na hadithi ngumu sana ambayo sipendi kuirudia. Nilimchukua kutoka  nyumba ya watoto ambayo nilikuwa Mathare. Kabla hata aletwe kwa Children’s Home, ana hadithi ya kuhuzunisha sana. Kwa hiyo, hata kama nyie mnaandika kwa ajili ya kupata likes na views, tuwe na utu. Hawa ni watoto maalum," alisema.