Wizkid aonekana mwenye huzuni wakati wa kuwasha mishumaa kuaga marehemu mamake (video)

Wizkid akiwa kwenye tsheti nyeusi, alionekana mnyonge na alishikilia mshumaa shingo upande huku akiwa amepotea kwenye lindi la mawazo ya huzuni.

Muhtasari

• "Wizkid ameumia sana, Mungu ampe ujasiri wa kuendelea." Mwingine alibaini.

• Bi Jane Dolapo Balogun alifariki mwendo wa saa 1.30 asubuhi siku ya Ijumaa Agosti 18

Wizkid afiwa na mamake
Wizkid afiwa na mamake
Image: Insta

Wanasema uchungu wa kufiwa na mama mzazi ni jambo ambalo linaweza likamnyong’onyeza hata mwanamume mzima na midevu yake.

Ikiwa ni Zaidi ya mwezi mmoja tangu mamake msanii nguli wa Afrobeats Wizkid alipofariki, marehemu angali bado kuzikwa.

Mamake Wizkid anatarajiwa kuzikwa Ijumaa Oktoba 13 na Jumatano usiku familia ya Wikzid iliandaa hafla ya kuwasha mishumaa kuonesha heshima za mwisho kwa mtu ambaye Wizkid alimtaja kama nguzo ya mafanikio yake ya kimuziki.

Video kutoka kwa tukio hilo imewaacha wengi katika hali ya simanzi.

Wizkid ambaye alikuwa mmoja wa wanafamilia walioshiriki katika kuwasha mishumaa kwa ajili ya marehemu alikuwa amevalia tsheti ya rangi nyeusi kama wengine na mshumaa uliowashwa mkononi.

Msanii huyo alionekana mnyonge na aliyezama kwenye lindi la mawazo na huzuni kutanda kwenye uso wake alionekana mwenye kutojua kilichokuwa kikiendelea wakati wenzake wanacheza kwa nyimbo za kufariji.

Video hiyo iliwafanya mashabiki wake kuweza kutambua kwa haraka bila kuambiwa kwamba msanii huyo kweli alikuwa amehuzunika kwa kupoteza hazina kuu katika maisha yake.

“Pole sana Wizkid, kusema kweli unaonekana mnyonge sana, siwezi jiweka katika kile ambacho kinaendelea katika kichwa chako lakini kubali pole zangu,” mmoja aliandika.

"Wizkid ameumia sana, Mungu ampe ujasiri wa kuendelea." Mwingine alibaini.

Bi Jane Dolapo Balogun alifariki mwendo wa saa 1.30 asubuhi siku ya Ijumaa Agosti 18 katika tukio la kushtua ambalo limeiweka tasnia ya burudani katika hali ya maombolezo.

Kifo cha Balogun kilithibitishwa na meneja wa msanii huyo, Sunday Aare, ambaye alisema mamake Wizkid alifariki asubuhi ya Ijumaa.

Marehemu Bi. Balogun, alikuwa nguzo ya usaidizi katika taaluma ya muziki yenye mafanikio ya mwanawe.