“Mboka ilizima hivi!” Karen Nyamu afunguka jinsi babake alivyomzuia kuwa Miss Kenya

Seneta Nyamu alidai kuwa waandalizi wa shindano hilo walikuwa na hakika kwamba angeshinda.

Muhtasari

•Karen alifichua kwamba alipokuwa akifanya masomo yake ya sheria alitafutwa kwa Shindano la Urembo la Kenya.

•Ndoto ya Karen ilidumu hadi baba yake alipomtaka achague kati ya kuendeleza masomo yake na uanamitindo.

Image: FACEBOOK// KAREN NYAMU

Seneta wa kuteuliwa, Karen Njeri Nyamu amefichua kwamba alijihusisha na uanamitindo wakati fulani katika siku zake katika Shule ya Sheria ya Kenya.

Siku ya Jumanne asubuhi, mwanasiasa huyo wa UDA alifichua kwamba alipokuwa akifanya masomo yake ya sheria katika Shule ya Sheria, alitafutwa kwa Shindano la Urembo la Kenya.

Karen alisema kuwa alihudhuria masomo ya uanamitindo kwa lengo la kushinda shindano hilo na kudai kuwa waandalizi walikuwa na hakika kwamba angeshinda.

“Nikiwa katika shule ya sheria nilitafutwa kwa shindano la urembo la Miss Kenya. Kwa sababu ya urefu wangu na viunga vya kiuno vya kupinda, Chris Kirwa na timu yake walishawishika kuwa wamepata mshindi wa mwaka huo. Nilichukua masomo ya uanamitindo ambapo nilijifunza kutembea huku nikikunja viuno hivi,” Karen Nyamu aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook na kuambatanisha taarifa hiyo na picha yake akiwa amesimama kama mwanamitindo.

Ndoto ya mama huyo wa watoto watatu ilidumu hadi wakati baba yake, Bw Nyamu alipomtaka achague kati ya kuendeleza masomo yake na uanamitindo.

"Mwishowe Bw Nyamu aliniambia nichague kati ya shule na upuuzi😆 Mboka ikazima hivo," alisema.

Mpangaji wa hafla maarufu Chris Kirwa alithibitisha kwamba kwa hakika mwanasheria huyo aliibuka bora wakati wa kuwasaka washindani wa Miss Kenya, akidokeza kuwa alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda shindano hilo.

Mapema mwake huu, seneta Nyamu alifichua katika mahojiano kwamba alikulia katika familia ya Kikristo iliyoongozwa na maadili makali.

Alifichua kwamba wazazi wake na ndugu zake wanne walikuwa wameokoka na watu wanaokwenda kanisani, jambo lililomfanya kuwa mtoto mwenye nidhamu.

"Sijawahi kuwa mtukutu sana. Sikuwa na ushirika mbaya. Nilikuwa mtu wa kanisa kwa sababu tumelelewa kanisani. Hata marafiki niliowajua walikuwa washiriki wa brigedi, washiriki wa kundi la vijana wa kanisa na vikundi vya densi vya kanisa,” alisema katika mahojiano na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume na Ene..

Aliongeza, “Bado nimeokoka, nampenda Mungu. Mtu hawezi kufika nilipo bila msingi wa neno la Mungu.”

Bi Nyamu pia aliweka wazi kuwa tangu ujana wake alitaka kuwa wakili na akafichua alitaka kuwa kama kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua ambaye anasema alimuona kama kielelezo.