Akothee atangaza nafasi kadhaa za kazi wizara ya elimu ikitambua na kusajili shule yake

Nafasi hizo ni mkuu wa shule, mratibu wa fedha, katibu, walimu wa kutoka chekechea hadi gredi ya 6, waongozaji wa masomo ya kuogelea, wapishi, walezi wa watoto, wasafishaji na nesi.

Muhtasari

• “Leo ndio siku ambayo nimehisi athari kubwa zaidi ya Chanya katika maisha yangu. AKOTHEE ACADEMY SASA IMESAJILIWA KIKAMILIFU chini ya Wizara ya Elimu.," alisema.

Akothee
Akothee
Image: Instagram

Msanii na mjasiriamali Esther Akoth maarufu kama Akothee ni mfanyibiashara mwenye furaha ambaye ameishi kuona ndoto yake ya muda mrefu ikitimia – ndoto ya kuanzisha shule ili kutoa elimu kwa familia za kimaskini.

Akothee hivi majuzi alitangaza kwamba hatimaye wizara ya elimu ilitambua na kusajili shule yake, ikiwa ni ishara ya kibali kuendelea kutoa masomo kwa jamii za kimaskini kupitia academia ya wakfu wake

Akipakia picha akiwa ameshikilia cheti cha kusajiliwa kwa shule yake na wizara ya elimu, Akothee alisema kwamba hiyo ndio siku ambayo alihisi ukubwa wa aina yake kwani hatimaye ndoto yake katika jamii itapata nuru na mwanga wa kufanikisha kile ambacho mwenyewe hakuweza kukipata akiwa mdogo.

“Leo ndio siku ambayo nimehisi athari kubwa zaidi ya Chanya katika maisha yangu. AKOTHEE ACADEMY SASA IMESAJILIWA KIKAMILIFU chini ya Wizara ya Elimu. Niruhusu nimshukuru Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti Bw Jacob Oyiego pamoja na timu yake. Kwa msaada wake mkubwa. Nasema Ahsante Sanaaaaa Sir,” Akothee alisema.

Hatua hii inakuja siku chache tu baada ya Akothee kutangaza nafasi kadhaa za kazi katika shule hiyo akisema kwamba hiyo ni kuenda chini katika historia kuwa mwaka huu utakumbukwa kwake kwa kuandikisha historia mpya.

Miongoni mwa nafasi za kazi alizozitangaza ni mkuu wa shule, mratibu wa fedha, katibu, walimu wa kutoka chekechea hadi gredi ya 6, waongozaji wa masomo ya kuogelea, wapishi, walezi wa watoto, wasafishaji na nesi.

Akitangaza nafasi hizo, Akothee alisema ni njia moja pia ya kurudisha mkono katika jamii ambayo imemshikilia kwa muda ili kufanikisha ndoto yake, akisema kwamba aliamua kuingilia suala la elimu baada yake mwenyewe kutaabika bila elimu alipoachia shule njiani kwa sababu ya ukosefu wa karo.

“Hatimaye naweza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuufanya mwaka wa 2023 kuwa mwaka wa kurejea tena, mwaka ambao umenipa furaha nyingi sana. Akothee Foundation Academy imekuwa kwenye orodha yangu ya ndoo tangu nilipoacha shule na nikaona jinsi nilivyokuwa nisiyefaa niliposhindwa kumudu ada ya shule kwa watoto wangu 🙏. Ningependa kutoa fursa hii kwa jamii yangu na taifa kwa ujumla, kusaidia na kuwezesha Jumuiya yangu,” alisema.