(Video) Jinsi Sonko alitumia zaidi ya Sh1M kwa vileo kusherehekea birthday ya Uhuru Kenyatta

Mhudumu wa duka hilo la vileo alifichua kwamba Sonko alinunua pombe yenye thamani ya shilingi milioni moja na elfu 29.

Muhtasari

• Kabla ya kulipia, Sonko alisimama mbele ya kamera na kumuimbia wimbo Uhuru Kenyatta wimbo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa.

Sonko amsherehekea Uhuru Kenyatta
Sonko amsherehekea Uhuru Kenyatta
Image: Twitter

Unaambiwa mwenye pesa si mwenzio, mpishe apite!

Wakati Wakenya wengi wanalalamika vikali kuhusu gharama ya juu ya maisha, kwa aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko hizo ni hekaya tu za Abunuwasi.

Mfanyibiashara huyo kwa mara nyingize alionesha ubabe wake wa kifedha baada ya kutumia Zaidi ya shilingi milioni moja katika vileo ili tu kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta.

Sonko katika mtandao wake wa X, awali ukifahamika kama Twitter wikendi iliyopita alipakia video akionesha jinsi aliingia katika duka moja la kuuza vileo na kuchagua pombe ainati zenye bei ghali ambapo baadae alilipia.

Kabla ya kulipia, Sonko alisimama mbele ya kamera na kumuimbia wimbo Uhuru Kenyatta wimbo wa kusherehekea siku ya kuzaliwa.

Pia katika maandishi kwenye video hiyo, Sonko alifichua kwamba Uhuru alikuwa ni rafiki wake miaka ya nyuma lakini walikuja kukosana wakati wa kung’atuliwa kwake madarakani kama gavana.

Hata hivyo, alipokuwa akimtakia Uhuru heri njema ya kufikisha miaka 62, alimwmabia kwamba amemsamehe kwa yote mabaya ambayo aliwahi mfanyia.

“Nampongeza Rais Mstaafu Uhuru Muigai Kenyatta. Mola Mwema akupe afya njema na maisha marefu unapoadhimisha miaka 62 ya kuzaliwa kwake. Nimekupa zawadi ya keki, kadi, na vinywaji bora zaidi kama ishara ya kukosa siku za furaha tulizozoea kutumia pamoja kabla na baada ya kuwa rais. Heri ya siku yako ya kuzaliwa, kaka yangu, na mwaka wako wa ziada ukuletee furaha,” alisema.

“Mungu anisamehe kwa matusi, maneno yasiyofaa, na chochote nilichosema ili kukuchochea ulipize kisasi. Pia nimekusamehe kwa makosa na mateso yote. Uishi muda mrefu. Mungu akubariki wewe na familia yako,” aliongeza.

Mhudumu wa duka hilo la vileo alifichua kwamba Sonko alinunua pombe yenye thamani ya shilingi milioni moja na elfu 29.