Diamond awapa ushauri wasanii wenye ndoto za kuwa wanamuziki

Malengo yangu ya kununua ndege ya kibinafsi ni kuwapa motisha vijana kwamba yote yawezekana.

Muhtasari

• Nyota huyo wa Bongo alisema haya baada ya kutua uwanja wa ndege Kahama nchini Tanzania baada ya kukamilisha ziara yake ya siku mbili mjini Nairobi kwa Tamasha la Oktobafest.

Diamond Platnumz.
Diamond Platnumz.
Image: Screengrab

Staa wa Bongo Diamond Platnumz ametoa ushauri kwa vijana wenye nia ya kujitosa katika ulingo wa muziki kuhimili changamoto katika taaluma hiyo.

Diamond alisema kuwa fani ya muziki inachangamoto za aina yake kama vile matusi na kukejeliwa kuwa hujui kuimba au sauti yako haivutii.

"Mimi kwa maisha yangu naamini kwamba kila kitu kinawezekana ukimuamini Muumba wako vijana wengi wanatamani kuwa kama mimi ila kuna changamoto nyingi  ushauri wangu ni mfanye kazi kwa bidii...".

"Cha muhimu ni vijana mkumbali changamoto ambazo ni kibao kwa wanamuziki mfano mimi wengi walinikejeli kuwa mimi sijui kuimba, wengi wakanitusi wakisema mimi si mwanamuziki ila nilijipa moyo na kumuomba Muumba wangu anipe ujasiri", alisema msanii Diamond.

Nyota huyo wa Bongo alisema haya baada ya kutua uwanja wa ndege Kahama nchini Tanzania baada ya kukamilisha ziara yake ya siku mbili mjini Nairobi kwa Tamasha la Oktobafest.

Kwenye mahojiano ya moja kwa moja na mwanablogu wa Wasafi Media, msanii huyu alisema kuwa yeye hufanya bidii ili awape mfano mzuri wasanii wachanga kufanikisha vipawa vyao.

"Inachukua muda  kwa nyota ya mwanamuziki kunawiri, nilianzia mbali ndio maana nina lengo la kununua ndege ya kibinafsi kwa manufaa yangu na wananchi wa Tanzania ili kuonesha vijana kuwa yote yanawezekana kwa anayetia bidii", alisema msanii Diamond.