Akothee afichua kwa nini aliambatanisha harusi yake na siku yake ya kuzaliwa

"Nilifanya harusi yangu siku moja na ile yangu ya kuzaliwa, ili tu kwamba mambo yakienda mvange kama ambavyo yamekwenda, basi nitakuwa kwamba nilijibamba,” alisema.

Muhtasari

• "Ninataka kuwapa habari kwamba samahani, ni lazima tubebe mizigo yetu tuondoke kwa sababu haukuwa uhusiano,” aliongeza.

Akothee
Akothee
Image: Instagram

Mjasiriamali Akothee kwa mara ya kwanza amezungumzia yale ambayo watu wengi hawakuwa wanajua kuhusu ratiba ya harusi yake mwezi Aprili na mpenzi wake Mr Omosh.

Akizungumza na mashabiki wake katika kipindi cha moja kwa moja kwenye ukurasa wake wa Facebook usiku wa Jumanne, msanii huyo tajiri alisema kwamba hata kabla ya harusi yake, alikuwa na hisia nyingi tu kwamba ndoa yake baada ya harusi haingedumu.

Kutokana na hisia hizo, Akothee alisema kwamba alihakikisha siku yake ya harusi inaambatana na siku yake ya kuzaliwa ili likitokea la kutokea basi asije akajuta kwamba alifanya tafrija na sherehe ya kukata na shoka kwa kitu kilichofeli.

Alisema kwamba kilichomsukuma kuwekeza pakubwa katika siku hiyo ya Aprili 30 ni kwamba ilikuwa pia ndio siku yake ya kuzaliwa, kwa maana kwamba hata kama ndoa ingevunjika baadae – kitu ambacho kilikuja kutokea miezi 5 baadae – basi asingejuta kwa sababu angejiliwaza kwamba uwekezaji ule ulikuwa ni kwa ajili ya siku yake ya kuzaliwa.

“Mimi ni mtu ambaye anachukua tahadhari. Kusema ukweli nilijifurahisha na kujibamba katika ndoa yangu. Nilifurahia harusi yangu na huwa sijutii kitu chochote, sijutii hata kidogo. Na ili kuweka mambo wazi, nilifanya harusi yangu siku moja na ile yangu ya kuzaliwa, ili tu kwamba mambo yakienda mvange kama ambavyo yamekwenda, basi nitakuwa kwamba nilijibamba,” alisema.

“Na ninataka kumshukuru kila mtu ambaye alijitoa kimawazo, kifedha… watu wengi waliwekeza katika harusi ile, wengine waliwekeza katika muunganiko wetu lakini sasa ninataka kuwapa habari kwamba samahani, ni lazima tubebe mizigo yetu tuondoke kwa sababu haukuwa uhusiano,” aliongeza.