Madaktari walazimika kuukata mguu wa Mr Ibu ili kuokoa maisha yake

“Kufikia saa saba mchana, mchana wa leo, Baba amefanyiwa upasuaji mara 7, lakini ili kumuweka hai na kuongeza uwezekano wa kupona, ilibidi mguu wake mmoja ukatwe.” taarifa ya familia ilisoma.

Muhtasari

• "Maendeleo haya yamekuwa magumu kwetu sote, lakini imetubidi tukubali kama ukweli mpya wa Baba ili kumuweka hai.” ripoti ya familia ilisema.

Mr Ibu
Mr Ibu
Image: Instagram

Taarifa mpya kutoka kwa familia ya mwigizaji John Okafor, almaarufu Bw Ibu ambaye amekuwa akiugua na kulazwa hospitalini kwa kipindi cha takribani mwezi mmoja, imefichua kuwa mguu wake mmoja umekatwa ili kumuweka hai.

Habari ziliibuka mnamo Oktoba kwamba mwigizaji huyo mkongwe alikuwa mgonjwa na alihitaji msaada wa kifedha kusaidia katika matibabu yake.

Katika taarifa hiyo iliyosambazwa kwenye ukurasa wa Instagram wa muigizaji huyo Jumatatu, ilifichua kuwa mwigizaji huyo alifanyiwa upasuaji mara saba, ikiwa ni pamoja na kukatwa mguu mmoja, kwa nia ya kumuweka hai.

Taarifa hiyo ilisomeka;

“Habari za mchana, Wanigeria. Tunataka kuthamini kila mtu ambaye amepitia kwa baba yetu; kusema tunashukuru ni jambo la kukanusha, na ni Bwana mwema pekee ndiye anayeweza kuwashukuru nyote vya kutosha kwa kila msaada ambao mmetoa.”

“Kufikia saa saba mchana, mchana wa leo, Baba amefanyiwa upasuaji mara 7, lakini ili kumuweka hai na kuongeza uwezekano wa kupona, ilibidi mguu wake mmoja ukatwe.”

"Maendeleo haya yamekuwa magumu kwetu sote, lakini imetubidi tukubali kama ukweli mpya wa Baba ili kumuweka hai.”

"Tafadhali, bado tunaomba usaidizi kutoka kwa Wanigeria wenye nia njema kwani, katika hatua hii, baba bado ni dhaifu sana, na anahitaji msaada wote anaoweza kupata.”

“Asante, kila mtu, familia ya Okafor inashukuru na hatuwachukulii kirahisi. Kwa wakati ufaao, Baba atamthamini kibinafsi kila mtu ambaye alimuunga mkono katika kipindi hiki mara tu atakapokuwa imara.”

Itakumbukwa awali tuliweza kuripoti kwamba baada ya mwigizaji huyo kufanya video akiwa katika kitanda cha hospitali na kuomba msaada wa hela za matibabu, watu mbali mbali wakiwemo wasanii walijitokeza na kuahidi kumkwamua.

Msanii Peter Okoye, maarufu Rudeboy kutoka kundi la muziki la PSquare aliwarai wenzake kina Davido kujitokeza ili kumsaidia jamaa huyo ambaye alimtaja kuwa kiburudisho kwenye runinga kwa muda mrefu.