Harmonize aguswa na video ya jamaa akiendesha baiskeli usiku, aahidi kumnunulia pikipiki

"Endapo post yangu ikikufikia basi nitafute nikuchukulie hata Bodaboda,” Harmonize aliandika.

Muhtasari

• Kwa kujituma, jamaa huyo aliendesha baiskeli kwa kasi lakini akapitwa na gari la yule aliyekuwa akimrekodi.

Harmonize
Harmonize
Image: Instagram

Harmonize ameoneshwa kuguswa kwake na video ya jamaa ambaye alirekodiwa kutoka ndani ya gari lake akiendesha baiskeli kwa kasi mida ya usiku.

Msanii huyo wa Konde Music Wordwide alipakia video hiyo ambayo ilirekodiwa na mtu aliyekuwa ndani ya gari katika barabara moja akiwa anang’ang’ana kuiendesha kwa kasi ili pengine kuwahi nyumbani baada ya kazi.

Kwa dalili zote, mwendesha baiskeli huyo alikuwa ni kama mtu anatoka sokoni baada ya kuuza bidhaa zake, kwani nyuma alikuwa amefunga kapu kubwa na katika pande zote mbili alining’iniza gunia za kubebea mizigo.

Kwa kujituma, jamaa huyo aliendesha baiskeli kwa kasi lakini akapitwa na gari la yule aliyekuwa akimrekodi.

Ni video ya kutia huruma sana ambayo ilimgusa Harmonize ka kuahidi kwamba endapo atafikiwa na habari zake, basi yuko radhi kukutana naye na hata kumnunulia pikipiki ili kuboresha maisha kutoka kwa baiskeli.

“Hii imenigusa sana, ahsante kaka, endelea kupambana na Mungu akufungulie milango ya riziki. Endapo post yangu ikikufikia basi nitafute nikuchukulie hata Bodaboda,” Harmonize aliandika kwenye video hiyo aliyoichapisha katika instastory yake.

harmonize
harmonize

Lakini pia kingine cha kuzungumzia kutoka kwa video hiyo ni kwamba kwa nyuma, alikuwa amening’iniza picha ya Harmonize na kuandika ‘Amelowa’ wimbo ambao alimuimbia Kajala kipindi bado penzi lao halijaingia mchanga.