Hata Harmonize aungane na Rayvanny bado hawamwezi Diamond - Mkubwa Fella

“Labda mimi nizimie, ila kwa sasa hivi wakati niko naye ni vigumu. Au labda mimi nisiwepo kwa sababu kuna leo na kesho,” alisema.

Muhtasari

• Pia katika mahojiano, Harmonize alimzungumzia kwa mazuri Alikiba akisema kwamba ni mmoja wa wasanii ambaye anajifunza mengi kutoka kwake kimuziki.

Harmonize na Rayvanny
Harmonize na Rayvanny
Image: maktaba

Meneja wa Diamond Platnumz, Mkubwa Fella amevunja kimya chake kuhusu msanii Harmonize hivi karibuni kuonekana kujenga ukaribu wake na Alikiba lakini pia na Rayvanny.

Harmonize aliporejea kutoka Marekani, alimletea Rayvanny tuzo yake ambayo Rayvanny mwenyewe aliifuata Konde Village na kukumbatiana na Harmonize wakitangaza Amani.

Pia katika mahojiano, Harmonize alimzungumzia kwa mazuri Alikiba akisema kwamba ni mmoja wa wasanii ambaye anajifunza mengi kutoka kwake kimuziki.

Jambo hili lilitafsiriwa na baadhi ya Mashabiki wa muziki kwamba ni njama ya kuungana ili kujenga timu ya kumng’oa Diamond katika kilele cha mafanikio ya kimuziki.

Akizungumza katika kituo cha East Africa Radio, Mkubwa Fella alifutilia mbali uwezekano wa wasanii hao kuungana na kumuangusha Diamond, akisema kwamba hawamwezi Diamond hata kidogo.

Mkubwa pia alisema kwamba wasanii Harmonize na Rayvanny wote walitokea chini ya mbawa zake na kukiri kwamba itakuwa vigumu kwao kumshinda Diamond.

“Hivi mnajua kwamba Rayvanny katokea Mkubwa na Wanawe? Pia huyo Rajab ameanza kutokea kwangu kabla ya kuenda WCB, maanake ninasema Harmonize. Lakini wakati huo anakuja anaitwa Harmonize, kwa hiyo wote wametoka kwenye koo yangu, ila kwa Diamond hawamwezi,” Mkubwa Fella alisema.

Alizidi kusisitiza msimamo huo akisema kwamba njia pekee ya wasanii hao kumshinda Diamond baada ya kuungana ni labda yeye asiwe meneja wa Diamond tena au awe hayupo duniani.

“Labda mimi nizimie, ila kwa sasa hivi wakati niko naye ni vigumu. Au labda mimi nisiwepo kwa sababu kuna leo na kesho,” alisema.