Sababu za Akothee kutoa zawadi za shilingi milioni moja kwa mashabiki wake

"Sihitaji zawadi, lakini nataka kuwapa. Nina KSh 1 milioni za kunyakuliwa. Ninataka kuwashukuru mashabiki wangu kwa kuwa waaminifu, na wanaonilinda na kunipigania hapa"," alisema.

Muhtasari

• Akothee ataanza kutoa zawadi za hadi shilingi milioni moja kwa mashabiki wake wote kuanzia Desemba 1.

Akothee
Akothee
Image: Facebook

Msanii na mjasiriamali Esther Akoth Kokeyo maarufu kama Akothee ametangaza kuleta mabadiliko mapya katika uhusiano wa wasanii na watu maarufu na mashabiki wao wanaowaunga mkono mitandaoni kila siku.

Akothee katika video moja ambayo inaenezwa mitandaoni alisema kwamba kuanzia Desemba hii, ataanza kutoa zawadi za shamrashamra za Krismasi mapema kwa mashabiki wake ambao wamekuwa wakimuunga mkono muda wote mitandaoni na kumfanya kuwa na ufanisi mkubwa si tu kama msanii lakini pia kama mjasiriamali.

Akothee ataanza kutoa zawadi za hadi shilingi milioni moja kwa mashabiki wake wote kuanzia Desemba 1.

Alisema hahitaji zawadi yoyote kutoka kwa mashabiki wake lakini anataka kuwarudishia kwa kuwa mwaminifu na kujihami.

"Kuanzia Desemba 1, nitakuwa na pesa. Nina KSh 1 milioni kwa mashabiki wangu wote. Unachohitajika kufanya ni kufuata maagizo tu. Sihitaji zawadi, lakini nataka kuwapa. Nina KSh 1 milioni za kunyakuliwa. Ninataka kuwashukuru mashabiki wangu kwa kuwa waaminifu, na wanaonilinda na kunipigania hapa… Hakikisha unanifuata kwenye TikTok, Facebook, Twitter na YouTube,” alisema.

Kinyume na ambavyo amekuwa akijitapa kwamba amejitengeneza na kujipaisha mwenyewe hadi kwa mafanikio yake kutokana na juhudi zake, Akothee alitengua kauli hiyo na safari hii kukiri kwamba kama si mchango mkubwa wa mashabiki wake, asingekuwa chapa ya kuaminika kama alivyo sasa hivi.

"Mmekuwa mkitoa maoni. Pambano letu lilikuweka kwenye hali ya kusisimua. Tunawafanya mpigane na watu mashuhuri. Tunawafanya mpigane na chipukizi. Unahusika kihisia katika chapa hii. Nadhani ni wakati muafaka wa kunizawadia pesa zangu. Nataka mnijaze kwenye mifuko yenu. Nyinyi watu mmenisaidia kujenga chapa hii. Siwezi kamwe kujivunia na kusema nimejitengeneza,” alisema.