Mbona Akothee avalie headphones wakati anatangamana na watu? - Robert Alai auliza

Alai alimkosoa Akothee kwa tabia hiyo ya kuvalia headphones wakati unaona watu wengi wamekuzingira wanataka kuzungumza na wewe, akisema kuwa sio picha nzuri kwa mtu mwenye ushawishi kama yeye.

Muhtasari

• "Kwa nini lazima uvae wakati unawasiliana na mtu wa kawaida? Akothee yawa!” Alai aliuliza.

Akothee akiwa na headphones zake.
Akothee akiwa na headphones zake.
Image: facebook

MCA wa Kileleshwa katika kaunti ya Nairobi, Robert Alai ameonesha kutoridhishwa kwake na mwenendo wa mjasiriamali Esther Akothee kuvalia headphones masikioni wakati anatangamana na watu.

Alai alichapisha picha ya Akothee akipokelewa na watu katika uwanja wa ndege huku katika masikio yake amevalia headphones na simu mkononi ishara kwamba alikuwa anasikiliza muziki.

Kwa kawaida mtu anapovalia headphones maskioni, ni vigumu sana kusikia kile ambacho watu wanamsemeza.

Alai alihisi kwamba kitendo cha Akothee kuvalia headphones wakati anakutana na watu ni kama kuwadharau watu hao kwani anaonesha kuwa hataki kuwasikiliza kile wanachomsemeza, japo pia ikumbukwe Akothee si mwanasiasa.

“Sio kwa ubaya, headphones ni kwa ajili ya kusikiliza Redio wakati wa kwenda au nini? Kwa nini lazima uvae wakati unawasiliana na mtu wa kawaida? Akothee yawa!” Alai aliuliza.

MCA huyo ambaye ni mkosoaji mkuu wa mitikasi ya Akothee muda wote alisema kwamba headphones zinafaa kuvaliwa pengine mtu akiwa anasafiri ndani ya ndege au gari lakini si kwenye hadhara wakati unajua kabisa watu wote wanaojitokeza kwa wingi kukutana na wewe wanataka kukupa ujumbe Fulani na wewe unaziba masikio usiwasikilize.

“Kwa ndege Sawa. Lakini hata kwa parking mko na hizi archaic pedhos?” aliuliza.

Tabia kama hiyo ya kuvalia headphones unapoingia kwa halaiki ya watu hushuhudiwa haswa kwa wachezaji wa soka.

Wachezaji wa soka wanapoingia uwanjani, kwenye njia wananyooshewa mikono na mashabiki lakini wao huishia tu katika kuwagusisha mikono haraka upesi wakipita pasi na kuwasikiliza huku masikio yao yakiwa yamezibwa na headphones.

Kwa muda mrfu, Alai amekuwa akitofautiana na Akothee katika mambo mengi tu ikiwemo kukejeli harusi yake ya mwezi Aprili ambayo ilikuja kubuma miezi 5 baadae, kuwa mstari wa mbele kupinga mwaliko wa Akothee kuwausia wanafunzi wa shule ya wasichana ya Ng’iya, mavazi yake miongoni mwa mengine mengi.