Ukivaa wigi linakuzeesha kwa miaka 14 zaidi ya umri wako - Wakili awaambia wanawake

"Weave juu ya kichwa chako inakufanya uonekane mzee zaidi ya miaka 7. Wigi hufanya mrembo kuzeeka miaka 14 zaidi ya umri wake halisi. Nywele fupi, za asili hupunguza umri kwa nusu,” Thuku alisema.

Muhtasari

•“Ni vile tu watu wengi wataogopa kukuambia hili ili kutuliza nafsi yako na hisia zako. Ukweli ni huo,” alisema.

Mawigi ya kichwani.
Mawigi ya kichwani.
Image: BBC NEWS

Jamaa mmoja anayetambulika kama wakili katika mitandao ya kijamii asubuhi ya Jumatano amezua mjadala pevu katika mtandao wa Facebook baada ya kulivalia njuga suala la wanawake kutumia nywele bandia vichwani mwao.

Wakili Wahome Thuku alitoa maoni yake kwamba wanawake wanaochagua kubaki katika nywele zao asilia huwa warembo Zaidi kulinganishwa na wenzao wanaotumia nywele bandia za kupandikiza tu.

Thuku alidai kwamba wanawake kutumia nywele za kusuka, kwa kimombo braids, huwafanya kuzeeka kwa mwaka mmoja Zaidi ya umri wao.

Lakini pia alidai kwamba wanaotumia nywele za kupandikiza, kwa kimombo weave, huwafanya kuonekana kuzeeka miaka 7 zaidi ya umri wako kamili na wale wa wigi huonekana wazee kwa miaka 14 zaidi ya umri kamili.

“TUWE wakweli. Misuko kichwani hukufanya uwe na umri wa mwaka mmoja zaidi. Weave juu ya kichwa chako inakufanya uonekane mzee zaidi ya miaka 7. Wigi hufanya mrembo kuzeeka miaka 14 zaidi ya umri wake halisi. Nywele fupi, za asili hupunguza umri kwa nusu,” Thuku alisema.

Alizidi kutema lulu akidai kwamba wanaume wengi wanapendelea warembo wenye nywele za kiasili lakini wanawapongeza tu wenye nywele bandia ili kuwapa hamasa tu lakini ukweli wa mambo ni kwamba nywele bandia hazivutii mwanamume hata kidogo.

“Ni vile tu watu wengi wataogopa kukuambia hili ili kutuliza nafsi yako na hisia zako. Ukweli ni huo,” alisema.

Aligusia pia kwamba hivi karibuni atagusia suala na wanawake kutumia kucha bandia na vipodozi vingine.

“Sijaguza kurefusha kucha bandia...nakuja huko muda si mrefu..😄” aliongeza.

Je, ni kweli wanaume wanavutiwa na wanawake wanaopenda kujiweka kwa urembo asilia bila kuchagiza kwa kutumia vipodozi?