Atwoli aongoza viongozi kusakata densi wimbo wa 'Tushangilie Kenya' wa Thomas Wesonga

Atwoli, Murkomen, Jalang'o, Sakaja, Ichung'wah walionekana kupungwa na wimbo huo na kuviacha viti vyao huku wakicheza densi na kupiga makofi Thomas Wesonga akihanikiza uwanja mzima.

Muhtasari

• Katibu mkuu wa chama cha wafanyikazi COTU, Francis Atwoli aliwaongoza viongozi wengi kuinuka na kuviacha viti.

Viongozi wakiserebuka na wimbo wa Thomas Wesonga.
Viongozi wakiserebuka na wimbo wa Thomas Wesonga.
Image: Screengrab//Live

Mwalimu Thomas Wesonga, Mkenya ambaye alileta mabadiliko makubwa katika utunzi wa nyimbo za kizalendo za Kenya tangu enzi za rais hayati Daniel Moi kwa mara nyingine tena ameonesha kuwa uzee ni dhahabu wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Kenya.

Thomas Wesonga alikuwa miongoni mwa kwaya na wasanii ambao walipata nafasi ya kutumbuiza wimbo alioutunga mwaka wa 1984 – Tushangilie Kenya – mbele ya umati wa watu wengi waliohudhuria sherehe za Jamhuri katika uwanja wa Jamhuri, eneobunge la Lang’ata.

Wasanii wengi walitangulia kutumbuiza na kuimba kwa mbwembwe lakini ilipofika zamu ya Thomas Wesonga na kwaya yake, wimbo wa ‘Tushangilie Kenya’ uliwazuzua na kuwafurahisha wengi.

Wimbo huo ulipozidi kunoga, viongozi wengi walijikuta wameinuka bila kuridhia na kuanza kusakata densi wakiimba pamoja na Wesonga.

“Tushangilie Kenya taifa letu tukufu, Kenya tunayoipenda daima …Kenya kipenzi chetu, hatutaiacha milele daima… mimi ni mwenye Kenya daima… …” sehemu ya mishororo ya wimbo huo wa kizalendo ilirindima na kuhanikiza katika uwanja wa Uhuru Gardens.

Mwalimu Thomas Wesonga,
Mwalimu Thomas Wesonga,

Katibu mkuu wa chama cha wafanyikazi COTU, Francis Atwoli aliwaongoza viongozi wengi kuinuka na kuviacha viti vyao kufurahia densi ya wimbo huo huku wakiimba kwa furaha kwa kujipata kuwa wao ni wazalendo wa Kenya.

Wengine ambao walionekana kuviacha viti vyao kwa densi ya wimbo huo wakipiga makofi ni pamoja na waziri wa barabara, ujenzi na miundombinu Kipchumba Murkomen, gavana Johnson Sakaja na naibu wake, mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor, waziri wa fedha Njuguna Ndung’u miongoni mwa wengine bila kumsahau kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah na waziri wa utalii Alfred Mutua.