Jamhuri Dei: Wakali wa Necessary Noize, Wyre na Nazizi waungana tena kwenye wimbo

Wanamuziki wengine ni pamoja na Gilad Millo, Fena Gitu, Bensoul, Kevin Bahati na Karwirwa Laura.

Muhtasari

• Wanamuziki wengine ni pamoja na Gilad Millo, Fena Gitu, Bensoul, Kevin Bahati na Karwirwa Laura.

Wyre na Nazizi
Wyre na Nazizi
Image: Instagram

Kenya leo hii Jumanne Desemba 12 inaadhimisha miaka 60 tangu kujinyakulia uhuru kutoka kwa mkoloni na kuwa jamhuri rasmi.

Sherehe za Jamhuri Dei zitaongozwa na rais William Ruto katika uwanja wa Uhuru Gardens jijini Nairobi na timu nzito ya wasanii wa kibabe imejiandaa vilivyo kuwapakulia Wakenya burudani la kipekee kusherehekea miaka 60 ya uhuru.

Kinachowavutia Zaidi mashabiki wa muziki kutoka enzi za miaka ya 90 ni kwamba wanachama wa bendi iliyovuma sana mapema miaka ya 2000s, Necessary Noize, Wyre na Nazizi tena wanatarajiwa kuungana kwenye moja ya vibao vingi vya kizalendo ambavyo vimeratibiwa kutumbuizwa.

Wamepangwa kutumbuiza skits na nyimbo za pamoja ambazo zimeundwa mahususi kwa ajili ya sherehe za Jamhuri Day.

Maonyesho hayo yalitayarishwa na Tume ya Kudumu ya Muziki ya Rais.

Itakumbukwa kwamba Wyre na Nazizi kila mmoja aliamua kujifanyia kazi zake za kimuziki takribani miaka 11 iliyopita baada ya kuteka anga kwenye bendi ya Necessary Noize na vibao vilivyohanikiza mapema miaka ya 2000s kama vile Kenyan Gal; Kenyan Boy, Bless Ma Room, Msenangu miongoni mwa vingine vilivyotajwa kuwa kama kauli za mitaani.

Hata hivyo walirudi pamoja kidogo tu mwaka 2022 lakini hawakuweza kuwapakulia mashabiki wao burudani na mbwembwe iliyotarajiwa, ila safari hii watakiwasha mubashara katika sherehe za Jamhuri.

Wengine wanaotarajiwa kutumbuiza ni pamoja na mwanamuziki Eric Wainaina ambaye anafahamika kwa mchanganyiko wake wa Benga ya Kenya inayotambulika kwa miondoko ya gitaa ya Soukouss, uelewano wa pop na ala za kitamaduni.

Nyimbo zake za mwanzo, Daima na Nchi Ya Kitu Kidogo zikawa wimbo wa taifa ambao umeimbwa nchi nzima.

Wanamuziki wengine ni pamoja na Gilad Millo, Fena Gitu, Bensoul, Kevin Bahati na Karwirwa Laura.

Kutakuwa na ushirikiano wa wimbo unaoitwa Kidete utakaochezwa na Bensoul, Bahati, Fena, Laura na Maimooh.

Wimbo unaoitwa Champion ameshirikiana na wasanii mbalimbali wakiwemo Nazizi, Wyre, Gilad na Johny Skani.