Samidoh awaacha mashabiki njia panda kwa kuimba wimbo wa kujutia maamuzi ya awali

“Ni lazima nifanye U-Turn, ni lazima nikengeuke, kwa sababu nilikuwa naelekea katika njia isiyofaa, nimeamua kuanza upya tena, ni lazima nifanye U-Turn…” sehemu ya wimbo huo ilikariri.

Muhtasari

• Wengi walihusisha maudhui ya wimbo huo na kile kinachokisiwa kuendelea katika maisha ya kimapenzi ya msanii huyo na kina mama kwa wanawe.

Samidoh.
Samidoh.
Image: TikTok

Msanii Smwel Muchoki maarufu kama Samidoh kwa wapenzi wa muziki wa Kikuyu, Mugithi amewaacha mashabiki wake na wale wanaolivalia sakata la maisha yake ya kimapenzi katika njia panda baada ya kurekodi video akifurahia wimbo wenye maudhui ya kujutia maamuzi ya awali.

Msanii huyo alipakia video hiyo kwenye ukurasa wake wa TikTok akiwa ndani ya gari na alijirekodi akifurahia kwa mbwembwe wimbo wa King George akimshirikisha P2K Dadiddy maarufu kwa jina ‘U-Turn’.

Kilichowachanganya wengi ni maudhui ya wimbo huo ambao unaashiria mtu ambaye amejuta kuhusu maamuzi ya awali na baada ya kugundua kakosea, ameamua kuchukua uamuzi mpya wa ghafla ili ujirudi kama njia moja ya kujirekebisha.

“Ni lazima nifanye U-Turn, ni lazima nikengeuke, kwa sababu nilikuwa naelekea katika njia isiyofaa, nimeamua kuanza upya tena, ni lazima nifanye U-Turn…” sehemu ya wimbo huo Samidoh alikuwa anasikiliza akijibamba nao uliimba.

Wengi walihusisha maudhui ya wimbo huo na kile kinachokisiwa kuendelea katika maisha ya kimapenzi ya msanii huyo na kina mama kwa wanawe, Edday Nderitu na Seneta maalum Karen Nyamu.

Samidoh na Nyamu wamekuwa wakihanikiza kote kote kulianika penzi lao kwa kila mtu kuliona na kulililia ngoa baada ya mke wa kwanza, Edday Nderitu kuweka wazi kwamba hakuwa na nia ya kushiriki penzi katika ndoa ya mitala – na hivyo kumuachia Karen Nyamu kipande chote cha mkate.

Lakini pia wiki iliyopita kulikuwa na uvumi mitandaoni kwamba Karen Nyamu na Samidoh penzi lao limeingia mchangani baada ya wadadisi kubaini wawili hao wamesitisha urafiki wao katika mtandao wa Instagram kwa kuacha kufuatana.

Tukio hilo limeoanishwa moja kwa moja na maudhui ya wimbo huo ambapo baadhi wanahisi Samidoh pengine anajuta kumkubali Nyamu huku akiteketeza penzi la mkewe Edday Nderitu ambaye sasa ni kama ndege aliyeponyoka mikononi mwa msasi na kumuachia manyoya tu.

Wengine walihisi kusema anajirudi na kuanza upya ni kama anapanga kujinyenyekeza kwa Edday kwa ajili ya msahama akiwa na nia ya kuirejesha familia yake ya watoto watatu ambao wote walihama na mama yao kwenda Marekani na tayari wameshaanza shule katika taifa hilo.