Meneja wa Diamond afichua WCB Wasafi wamo mbioni kumsaini Aslay

Tamko hilo linakuja miezi 3 tu baada ya Aslay kukanusha uvumi uliokuwa unamhusisha na kujiunga WCB Wasafi, akisema sasa hivi yuko na malengo yake tofauti.

Muhtasari

• "Na ndio sasa hivi nafanya mpango naongea na Naseeb [Diamond] Mungu akijaalia yule Aslay ampe shavu kidogo," alisema.

Aslay na Diamond
Aslay na Diamond
Image: Screengrab

Meneja wa lebo ya muziki inayomilikiwa na Diamond Platnumz, WCB Wasafi, Mkubwa Fella amefichua kwamba kuna mipango kabambe ya kumsaini msanii Aslay Isihaka katika lebo hiyo kubwa Zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika stesheni ya Wasafi FM, Fella alifichua kwamba Aslay ni moja ya wasanii wenye tajriba kubwa sana kimuziki lakini pia talanta ya kupigiwa mfano.

Fella alisema kwamba kwa sasa yuko kwenye mazungumzo ya kina na Diamond Platnumz kuhakikisha kwamba Aslay anasainiwa katika lebo ya WCB.

“Waakti Mbosso aliondoka Yamoto kujiunga na WCB Wasafi, nilitoa Baraka zangu zote na Diamond ndiye alikuwa mstari wa mbele kumpokea. Na ndio sasa hivi nafanya mpango naongea na Naseeb [Diamond] Mungu akijaalia yule Aslay ampe shavu kidogo, ni kijana ana talanta kubwa sana,” Mkubwa Fella alifichua.

Kauli hii ya Mkubwa Fella ambaye alimkuza Aslay tangu akiwa mdogo hadi anakuja kuongoza kundi la Yamoto bendi na hatimaye kusambaratika inakuja miezi michache tu baada ya Aslay kukanusha uvumi wa kujiunga na WCB Wasafi.

Katika mahojiano ya kipindi cha Amplifaya cha Clouds FM na Millard Ayo miezi mitatu iliyopita, Aslay alikanusha kuwepo kwa uvumi huo, akisema kwamba kwa bahati mbaya sasa hivi ashaingia kwenye lebo ya Rockstar ya Afrika Kusini na hana mpango wowote wa kuingia Wasafi.

“Diamond ni mtu mkubwa, ana uwezo wa kufanya kitu chochote na kwa wakati wowote na kikawa kikubwa. Kwa hiyo kutamani kunisaini WCB kwa sasa hivi hapana. Tayari nina malengo yangu na nina vitu vyangu ninavyotarajia kuvifanya. Lakini sijawahi fuatwa na Diamond kwamba anataka kunisaini wala watu wake hawajawahi nifuata,” aliongeza.

Lakini pia Aslay alikiri kwamba endapo kitatokea kitu chochote kwenye mzunguko wa maisha ya Sanaa basi yuko tayari kufanya kazi na msanii yeyote hata Diamond mwenyewe.