Msanii Bahati atoa ahadi ya kusaidia vijana kurekodi miziki na video Makueni

“Nimemfahamu Bahati kitambo. Ana roho nzuri." Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jr alimsifia.

Muhtasari

• Kiongozi huyo ambaye pia ni wakili alimsifia Bahati kwa kuwa na moyo wa kusaidia akisema kwamba amemjua kwa muda sasa kama mtu ambaye ana moyo mzuri.

Mutula Kilonzo awakaribisha Bahati na Diana ofisini mwake.
Mutula Kilonzo awakaribisha Bahati na Diana ofisini mwake.
Image: Facebook//Mutula Jilonzo Jr

Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jr amefichua kuwa wameafikiana maelewano na msanii Kelvin Kioko maarufu kama Bahati katika kuanzisha mchakato wa kuwasaidia vijana katika kaunti hiyo ya Ukambani kujiendeleza kisanaa.

Kilonzo kupitia ukurasa wake wa Facebook alifichua haya kwa kupakia picha za mkutano waliokuwa nao yeye pamoja na Bahati na mkewe Diana Marua.

Kiongozi huyo ambaye pia ni wakili alimsifia Bahati kwa kuwa na moyo wa kusaidia akisema kwamba amemjua kwa muda sasa kama mtu ambaye ana moyo mzuri.

Mutua alisema kuwa Bahati ameshatoa ahadi ya kusaidia vijana chipukizi katika Sanaa kurekodi miziki na video zao na hivi karibuni watatoa mwafaka wa jinsi ya kufikia ahadi hiyo na kuifanikisha.

“Nimemfahamu Bahati kitambo. Ana roho nzuri. Alifanya ziara ya ghafla ofisini kwangu na akajitolea kusaidia vijana katika kurekodi muziki na video. Tutapanga tukio hivi karibuni,” Kilonzo aliandika.

Msanii huyo ambaye katika siku za hivi karibuni ameonekana kujikita Zaidi katika masuala ya kijamii na kutokea kwenye hafla za kisiasa amewafanya wengi kuhisi kwamba anajaribu kuweka misingi thabiti kujitosa kamili kwenye siasa.

Ikumbukwe katika uchaguzi mkuu wa 2022, Bahati aliwania ubunge wa Mathare kwa tikiti ya chama cha Jubilee lakini akabwaga hadi nafasi ya tatu nyuma ya mshindi kutoka ODM na nambari mbili kutoka UDA.

Mwishoni mwa mwaka jana, Bahati na mkewe pia walionekana na hata kutumbuiza katika hafla ya kilele cha kipute cha katibu mkuu wa UDA, Cleo Malala Super Cup kaunti ya Kakamega.