Steve Simple Boy afichua azimio kuu 2024 ni kuzungumza Kiingereza tupu bila kuchanganya

Licha ya kuonekana kung’ang’ana hadi kutokwa jasho akijieleza kwa Kiingereza, msanii huyo alisisitiza kwamba mwaka huu ataendelea kutumia lugha hiyo.

Muhtasari

• Hivi majuzi, Jalang’oo alimsifia pakubwa Stevo Simple Boy kama rapa bora kuliko marapa wengine.

• Jalang’oo alisema haya katika hafla ya kuzindua wimbo wa KRG aliomshirikisha Konshens kutoka Jamaika.

Stevo Simple Boy
Stevo Simple Boy
Image: Screengrab

Rapa Stevo Simple Boy amefichua kuwa moja ya maazimio yake makuu kwa mwaka huu wa 2024 ni kuzungumza Kiingereza pekee bila kuchanganya na lugha zingine.

Akizungumza na YouTuber Trudy Kitui, rapa huyo mwenye misamiati ya kuchekesha alisema kwamba ameamua kufanya hivyo kwa sababu ya kuwakumbatia mashabiki wake wote, wengine wakiwa ni wale ambao huwa hawaelewi Kiswahili.

Licha ya kuonekana kung’ang’ana hadi kutokwa jasho akijieleza kwa Kiingereza, msanii huyo alisisitiza kwamba mwaka huu ataendelea kutumia lugha hiyo ya wakoloni bila kubabaishwa.

“Mwaka huu ni Kiingereza pekee lakini wakati mwingine nitakuwa nazungumza Kiswahili lakini muda mwingi ni Kiingereza. Niliamua kufanya hivyo kwa sababu mashabiki wangu wanakuwa na wasiwasi ‘Stevo unaweza zungumza Kiingereza au la?’” Stevo Simple Boy alisema.

Msanii huyo aling’ang’ana kwa Kiingereza na kutoa baadhi ya malengo yake kwa mwaka huu akisema kwamba atalenga kufanya Zaidi kimuziki huku akimkandia KRG the Don kuwa si msanii.

Stevo alikubaliana mia fil mia na maneno ya mbunge Jalang’oo kwamba yeye anampiku KRG katika muziki.

“Ni ukweli mimi ndio msanii bora, mimi ndio mtu mcheshi Zaidi hapa nchini Kenya na ningependa kumshukuru mheshimiwa Jalang’oo ahsante sana,” Stevo alisema.

Hivi majuzi, Jalang’oo alimsifia pakubwa Stevo Simple Boy kama rapa bora kuliko marapa wengine.

Jalang’oo alisema haya katika hafla ya kuzindua wimbo wa KRG aliomshirikisha Konshens kutoka Jamaika.

KRG pia alitumia fursa hiyo kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.