Stephen Letoo atangaza tarehe ya harusi yake

Hata hivyo, msemaji huyo wa kongamano la wanaume aliwaacha wengi katika njia panda na maswali mengi kwani hakuweza kubaini idadi ya wanawake atakaofunga ndoa nao.

Muhtasari

• Katika bango hilo, Letoo alisema kwamba ni rasmi Jumamosi ya Aprili 20 atachukua mke katika uga wa kimichezo wa Ole Ntimama kaunti ya Narok.

STEPHEN LETOO
STEPHEN LETOO
Image: Facebook

Mwanahabari Stephen Letoo hatimaye yuko mbioni kuondoka katika banda la watu wasio na wapenzi.

Hii ni baada ya mwanahabari huyo mcheshi kuweka wazi kwamba mwaka huu anafunga harusi yake ambayo itakuwa wazi kwa umma kuhudhuria.

Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii, Letoo aliweka bango lililo na maelezo kuhusu harusi yake, ikiwemo tarehe na mahali ambapo harusi ya umma itafanyika.

Katika bango hilo, Letoo alisema kwamba ni rasmi Jumamosi ya Aprili 20 atachukua mke katika uga wa kimichezo wa Ole Ntimama kaunti ya Narok.

Akielezea aina ya mavazi yenye mvuto ambayo kila mtu anatakiwa kuvaa, Letoo alisisitiza kwamba kila atakayetaka kuhudhuria wala hatolipishwa kiingilio mradi tu amepiga vazi lenye asili ya Nigeria, Rwanda au hata Kimaasai.

“Mimi Stephen Letoo nawakaribisha kwa uwanja wa Ole Ntimama kaunti ya Narok kwa harusi yangu ya umma ambayo itakuwa ya kufana, mavazi yawe na Kinyarwanda, Nigeria au Kimaasai,” maandishi kwenye bango hilo yalisomeka.

Hata hivyo, msemaji huyo wa kongamano la wanaume aliwaacha wengi katika njia panda na maswali mengi kwani hakuweza kubaini idadi ya wanawake atakaofunga ndoa nao.

Itakumbukwa Letoo amekuwa mstari wa mbele kupigia upatu na debe uhusiano wa kimapenzi ambao kila mwanamume anastahili kuruhusiwa fursa ya kuoa wanawake Zaidi ya mmoja – ndoa za mitala.

Na hilo ndilo lilikuwa swali kubwa kutoka kwa wengi wa mashabiki wake ambao walitaka kupata maelezo Zaidi kuhusu harusi hiyo ya umma, haswa katika kipengele cha idadi ya wanawake wa kuwaoa siku hiyo.

Letoo kwa kujitetea, alisema kwamba maelezo Zaidi kuhusu siku yake kuu yatafuata kwani ndio mwanzo mkoko unaalika maua.