Govi wa Machachari afichua kilichomchochea kuanza kulea ndevu

“Kwa kweli ninashukuru sana kwa character ile [Govi] kwa sababu imenileta Baraka nyingi katika maisha yangu, lakini pia nina Zaidi ya kufanya katika maisha," alisema.

Muhtasari

• Hata hivyo, alitaka kutonukuliwa vibaya kwamba hapendi kuhusishwa na kipindi hicho kwenye runinga ya Citizen kilichompa umaarufu.

GOVI
GOVI
Image: INSTAGRAM//MALIK_LEMMY

Muigizaji Malik Lemmy, maarufu kwa jina la Govi ambalo alikuwa analitumia miaka kadhaa iliyopita wakati akiigiza katika kipindi cha Machachari amefichua sababu kuu ya kubadilisha muonekano wake na kuanza kulea nywele lakini pia ndevu.

Kupitia Instagram stories zake, Govi alisimulia kwamba aliamua mwenyewe kuanza kulea ndevu ili kupata muonekano tofauti wa kumfanya ajiondoke katika picha ya wanayemuona kama ‘Govi’ yule mtoto kwenye Machachari.

“Sababu iliyonifanya nianze kulea ndevu ni kwamba nilitaka watu wakome kunihusisha na character ambaye walikuwa wamezoea kwenye kipindi Fulani miaka kadhaa iliyopita. Nikiwa bila nywele na ndevu, sura yangu ya uso kama mtoto inakuja na hivyo kuwakumbusha watu kuhusu Govi,” alisema.

Hata hivyo, alitaka kutonukuliwa vibaya kwamba hapendi kuhusishwa na kipindi hicho kwenye runinga ya Citizen kilichompa umaarufu.

Govi alionesha faraja yake kwa kipindi kile na kukubali kwamba kupitia kwa Machachari, alipata kuwa Malik Lemmy wa sasa ambaye anazidi kuupiga mwingi katika tasnia ya uigizaji na kujiingizia kipato.

“Kwa kweli ninashukuru sana kwa character ile [Govi] kwa sababu imenileta Baraka nyingi katika maisha yangu, lakini pia nina Zaidi ya kufanya katika maisha kuliko tu kuhusishwa na character ile,” alisema.

Govi alikiri kwamba maisha yanakwenda mbio sana na katika umri wake wa miaka Zaidi ya 20, kubakia na muonekano wa character ile hauwezi kusaidia sana na kwamba ni sharti watu wajitambue na kuenda na mabadiliko.

“Katika umri wangu wa Zaidi ya miaka 20 na uso wa mtoto haiwezi kusaidia sana, kwa sababu muda unaenda pia haraka sana. Acha tuone jinsi itakavyokuwa,” Govi alisema.

govi
govi

Hata hivyo, aliwatania mashabiki wake kwamba alikuwa anataka kunyoa ndevu zake na nywele ili kurejesha sura yake ya kitoto cha miaka 16 lakini mwishoni akapakia picha akiwa amenyoa nywele tu na kutania kwamba umeme ulipotea alipokuwa bado hajanyolewa ndevu.

“Leo nataka kunyoa ndevu zangu na nywele kabisa. Nahitaji kuanza kuonekana wa miaka 16 tena…tulipofika kwenye ndevu, stima ilipotea, poleni sana wapenzi watazamaji,” Govi alitania.