Kwa nini Nuru Okanga ameingiwa na wazo la kuacha shule wiki mbili tu baada ya kudahiliwa?

Wiki mbili zilizopita wakati wa maandalizi ya kuingia sekondari, marafiki zake walimnunulia kalamu 200 na kumpa onyo ya kutorudi baada ya miaka minne na alama ya D.

Muhtasari

• Okanga amekuwa akigonga vichwa vya habari tangu mwaka jana ilipofahamika kwamba alikuwa mmoja wa waahiniwa wa KCPE.

NURU OKANGA
NURU OKANGA
Image: FACEBOOK

Mwanasiasa chipukizi ambaye ni mtetezi mkali wa sera za kinara wa ODM Raila Odinga, Nuru Okanga amefichua kwamba wiki mbili tu baada ya kuingia shule ya upili, tayari ameanza kuingiwa na wazo baya la kusitisha azma yake ya kuendelea na masomo.

Okanga kupitia ukurasa wake wa Facebook, alitoa wito kwa wahisani wema kujitokeza na kuipiga jeki safari yake ya masomo kwani tayari hajatulia shuleni lakini ameanza kuona ugumu wa kupata karo ya shule kama kizingiti kikubwa ambacho huenda kitaikatisha safari yake ya kupata cheti cha KCSE.

Aliwaomba watu kutumia huduma ya kununua mjazo wa simu ambayo ingemfaidi kwa njia moja au nyingine ili kuendelea kusalia shuleni.

“Nafikiria kuacha shule kwa kukosa karo, naomba mnisaidie kwa kununua mjazo wangu wa simu kupitia Nambari ya Playbill 158 158 | NAMBA YA AKAUNTI NAMBA YAKO YA SIMU...tulipe Ada ya shule,” Okanga alisema.

Okanga amekuwa akigonga vichwa vya habari tangu mwaka jana ilipofahamika kwamba alikuwa mmoja wa waahiniwa wa mwisho kabisa walioshiriki katika kuifunga historia ya mitihani ya darasa la nane KCPE ambayo imekuwa ikifanywa kwa kipindi cha miaka 38 iliyopita.

Hata hivyo, kipindi chote hicho mpaka matokeo kutolewa na waziri wa elimu, Okanga amekuwa msiri kuweka wazi alama aliyoipata katika mitihani hiyo ya kufunga ukurasa wa mtaala wa 8-4-4.

Wiki mbili zilizopita akiwa katika maandalizi ya kujiunga kidato cha kwanza, marafiki zake katika Bunge la Mwananchi huku Jacaranda walimnunulia baadhi ya bidhaa muhimu vya kujiunga sekondari vikiwemo kalamu na vitabu.

Okanga alikabidhiwa kalamu zipatazo 200 na kuonywa kwamba endapo atafeli katika mtihani wa KCSE miaka minne ijayo, basi afahamu fika kwamba hatakuwa mgeni wa mtu katika Bunge la Mwananchi.

“Hizi kalamu kuna vile utazitumia, kidato cha kwanza utatumia kalamu 20, kidato cha pili utatumia kalamu 50, kidato cha tatu utatumia kalamu 70…Nuru Okanga tunakuambia, venye unaenda kidato cha kwanza, ukirudi na D…” alielekezwa.