MCA Tricky alaumu ujio wa mitandao kama msumari wa mwisho kwenye jeneza ya uchekeshaji

Tricky anahisi kwamba wachekeshaji wengi walianza kutumia mitandao ya kijamii kujipatia japo kitu wakati wa janga la Korona na mitandao hiyo ilisababisha viwango vya ucheshi kudorora.

Muhtasari

• "Kwa hiyo kama mfanyibiashara yeyote kipindi cha Korona, sisi wachekeshaji tungekimbilia wapi? Ilitubidi tukimbie kwenye ni rahisi kuzalisha,” aliongeza.

Mchekeshaji wa Churchill.
MCA Tricky// Mchekeshaji wa Churchill.
Image: Screengrab//YouTube

Mchekeshaji MCA Tricky ametoa maoni yake kuhusu kile anahisi kimesababisha viwango vya sekta ya uchekeshaji nchini Kenya kudorora pakubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Akizungumza na wanablogu katika uzinduzi wa shoo yake ya ‘Tricky Comedy & Vibes’ mchekeshaji huyo aliyekulia chini ya mwanzilishi wa ucheshi wa kisasa Churchill alisema kwamba uchekeshaji ulirudi chini kwa viwango wakati wa ujio wa mitandao ya kijamii.

Tricky anahisi kwamba wachekeshaji wengi walianza kutumia mitandao ya kijamii kujipatia japo kitu wakati wa janga la Korona na mitandao hiyo ilisababisha viwango vya ucheshi kudorora.

“Maoni yangu ya kweli ni kwamba wachekeshaji wa stand-up tumelala. Mimi nasema ukweli. Wakati mitandao imekuja, juzi wakati tulianza kuona utumbuizaji kupitia mitandao ya kijamii wakati wa Korona, watu walikimbia huko kutumbuizia watu. Mitandao ilifanya wasanii wakuwe wazembe sana. Uzembe uliingia ndani na nje, haswa kwa wale wasanii ambao walikuwa wa stand-up,” MCA Tricky alieleza.

Mchekeshaji huyo ambaye pia ni mtangazaji katika kituo kimoja cha redio humu nchini aliendelea mbele kutoa maelezo yake kwa upanda kwa nini anahisi mitandao ilikuja kama njia rahisi ya kuua kile ambacho kilikuwa kimeanza kuzaa matunda nchini.

“Mitandao ilikuja kama njia rahisi ya kutumbuiza, hauhitaji gharama yoyote, inahitaji muda mchache tu kufanikisha – huwezi kulinganisha na muda wa maandalizi kwenye ukumbi. Kwa hiyo kama mfanyibiashara yeyote kipindi cha Korona, sisi wachekeshaji tungekimbilia wapi? Ilitubidi tukimbie kwenye ni rahisi kuzalisha,” aliongeza.

Tricky anahisi kwamba utumbuizaji wa mitandaoni unamfungia sana mtu na humpi uhuru wa kujieleza kwa hadhira yake kama ambavyo unaweza katika hadhira ya moja kwa moja kwenye jukwaa.

“Mimi niligundua kwamba utumbuizaji wa mitandaoni unanifungia na kunibana sana kama msanii. Ninachoweza kufanya ni mistari kidogo lakini pia nikasoma hadhira yetu, hadhira yetu ikikuona unatumbuiza pale mitandao inasonga mbele na mwingine mwenye anakuja,” alisema.