Mimi ni baba kwa watoto 5 lakini sijui umri wao - Embarambamba

"Yaani nikiimba nyimbo za Mungu, lazima nikuwekee vitu viwili vitatu hapo unacheka usiboeke kwa mtandao. Unajua hata Mungu anataka burudani,” Embarambamba alifafanua.

Muhtasari

• “Unajua mimi sijakaa na hawa watoto sana. Ni mimba halafu naenda injili, katika hii kazi ya mwenyezi Mungu huwezi kaa sana sana kwa nyumba." alisema.

Embarambamba
Embarambamba
Image: FACEBOOK

Msanii wa injili mwenye utata kutoka eneo la Gusii, Chris Embarambamba amewashangaza mashabiki wake baada ya kudai kwamba hajui umri wa watoto wake.

Embarambamba ambaye alikuwa anazungumza katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha redio humu nchini alifichua kwamba yeye ni baba kwa watoto 5 lakini hajui umri wa mtoto hata mmoja.

Msanii huyo ambaye amejipata chini ya shinikizo na ukosoaji mkali kutokana na wimbo wake wa ‘Niko Uchi’ alijitetea akisema kwamba yeye kazi yake ilikuwa imejikita Zaidi katika kuzalisha, na suala la kukariri umri wa watoto likasalia kuwa la mkewe.

“Nimeoa, niko na watoto 5 na mke mmoja. Nilifanya kimchezo tu nikajipata nina watoto 5 na mke ni mmoja anaitwa Vane Embarambamba. Yeye ndiye anafua zile nguo ambazo mnaona za matope,” Embarambamba alisema.

“Mtoto wangu wa kwanza hata sijui umri wake, lakini najua tu amefikia wapi kimasomo. Ameingia kidato cha kwanza. Lakini miaka sijui, unajua mimi nilikuwa nazalisha tu, sijajua miaka. Wa mwisho sijui kama ni miaka 4 ama nafikiri sijui ni 3,” aliongeza.

Msanii huyo alijitetea akisema kwamba muda mwingi ameutumia katika kueneza injili na hivyo hajapata muda mwingi wa kukaa na wanawe kama ambavyo mama anavyokaa nao.

“Unajua mimi sijakaa na hawa watoto sana. Ni mimba halafu naenda injili, katika hii kazi ya mwenyezi Mungu huwezi kaa sana sana kwa nyumba. Nafanyia Mungu kazi na pia najifanyia kwa sababu huko juu [mbinguni] hakuna duka kuu wala hakuna malaika anashuka kila wiki kuja kutuletea chakula, sisi ndio tunajituma wakati tunahubiri injili, tupate mapato na kurudisha sadaka kwa kanisa,” alieleza.

Embarambamba alitetea mtindo wake wa kueneza injili ambao umekuwa ukikosolewa kuwa ni hatarishi kwa maisha yake na watu wanaomzunguka.

“Vile nilianza kueneza hii injili, nilianza kuieneza kwa kutumia ucheshi, yaani nikiimba nyimbo za Mungu, lazima nikuwekee vitu viwili vitatu hapo unacheka usiboeke kwa mtandao. Unajua hata Mungu anataka burudani,” Embarambamba alifafanua.