Familia ya Brian Chira yavunja kimya kufuatia ripoti za kifo chake katika ajali ya barabarani

"Sasa ameshaenda na inatupasa kupanga kila kitu. Husika hata kama alikuwa ni hasimu wako, Chira alikuwa kijana mzuri, najua wengi wanaumwa kama mimi lakini kila kitu kiko sawa" Mmoja alisema.

Muhtasari

• Ripoti za kifo cha Chira zilizagaa mitandaoni alasiri ya Jumamosi.

• Kulingana na Polisi waliozungumza na The Star Chira alifariki kutokana na ajali aliyohusika nayo, katika eneo la Karuri.

Brian Chira
Brian Chira
Image: Screengrab

Saa chache baada ya ripoti kuzaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha tiktoker Brian Chira kupitia ajali ya barabarani, familia yake imevunja kimya kuhusu ripoti hizo.

Baada ya kufika katika makafani ya City, jijini Nairobi alikolazwa Chira, wanafamilia hao walihakiki na kuthibitisha kuwa ni mwili wa Brian Chira.

Walithibitisha kwa wanahabari kwamba ni kweli Brian Chira ameshafariki dunia na kikubwa ambacho waliomba ni msaada wa kifedha kutoka kwa Wakenya ili kumpa buriani stahiki Chira lakini pia wakaomba maombi wakati wa kipindi  kigumu.

“Jumuiya ya TikTok, na mashabiki wake wote, ni kweli, Chira ameshatangulia mbele za haki. Amefariki na tafadhali tuombee kwa Mungu atupe nguvu. Tumefika hapa makafani na tumeona kile kilitokea, alihusika katika ajali mbaya ya barabarani, akaumia kichwa,” mmoja wa wanafamilia alisema.

“Naomba tafadhali tushirikiane kama mlimpenda Chira. Sasa ameshaenda na inatupasa kupanga kila kitu. Husika hata kama alikuwa ni hasimu wako, Chira alikuwa kijana mzuri, najua wengi wanaumwa kama mimi lakini kila kitu kiko sawa, ni lazima tumutumainie Mungu,” aliongeza.

Ripoti za kifo cha Chira zilizagaa mitandaoni alasiri ya Jumamosi.

Kulingana na Polisi waliozungumza na The Star Chira alifariki kutokana na ajali aliyohusika nayo, katika eneo la Karuri.

Inaarifiwa kuwa mwili wake ulikusanywa kutoka eneo la tukio Jumamosi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City mwendo wa saa tatu asubuhi.

Polisi walisema aligongwa na gari lililokuwa likienda kasi lakini hawana maelezo zaidi kuhusu hilo. Kulingana na gazeti la The Star, mwili wa Brian Chira umelazwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City ukiwa na majeraha kwenye paji la uso.

 

Polisi pia walisema marehemu alikuwa kwenye baa moja eneo la Gacharage na baadaye kusababisha zogo. Kisha alilazimishwa kutoka.

Baadaye alichukua pikipiki hadi nyumbani kwake na kushuka kabla hajajaribu kuvuka kwa miguu.

Lori la mwendo kasi lilimgonga na kuondoka kwa kasi. Haikusimama, mashahidi na polisi walisema. Suala hilo liko chini ya uchunguzi.

Taarifa za kifo chake zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakimuomboleza. Huku wengine wakiichukulia kama msukumo wa kufukuzia mbali na Tiktoker maarufu kwa sababu ya hatua alizochukua hapo awali.