Askofu mkongwe Timothy Njoya afichua jinsi alivyokutana na mkewe gerezani

“Nilikuwa nishaenda, niliona niko na Mungu mbinguni, nikafurahi sana. Nilikutana na Yesu, Malaika na watu wengi. Mbinguni ni furaha tu, haionekani na macho lakini inasikika. Malaika walikuwa wote ni Waafrika,” Njoya aliongeza.

Muhtasari

• Askofu huyo aliyefunga harusi na mkewe mwaka 1968 alifichua kwamba alimkuta kwa mara ya kwanza katika gereza la wanawake la Lang’ata.

Askofu Timothy Njoya
Askofu Timothy Njoya
Image: Screengrab//NTVKenya

Askofu mkongwe wa kanisa la PCEA Timothy Njoya amefichua kwamba alikutana na ubavu wake gerezani miaka kadhaa iliyopita kabla ya kufunga ndoa.

Njoya alifunguka maisha yake katika kitengo cha Masogora kweney runinga ya NTV wikendi iliyopita, ambapo kwa upana alielezea jinsi alikuwa akisawazisha maisha ya familia, kanisa na uanaharakati.

Askofu huyo aliyefunga harusi na mkewe mwaka 1968 alifichua kwamba alimkuta kwa mara ya kwanza katika gereza la wanawake la Lang’ata na kilichomvutia kwa mkewe huyo ni changamoto aliyompa baada ya kumsalimia.

“Mimi nilioa 1968, mimi sikuona kitu kizuri ama kibaya, nilijikuta tu nimezama kwenye penzi lake. Kwa sababu alinipa changamoto pale tulipokutana kwenye korokoro ya wanawake huko Lang’ata, nikaanza kuwasalimia nikiwanyesha upendo.”

“Nilifanya hivyo kuwaonyesha kwamba hawajapoteza kupendwa kwa sababu ya kuwa korokoroni. Wao ni watu, na ni binadamu na wanataka kupendwa, aliniambia hivyo. Akanihubiria, nikatubu nikaanguka, nikaokoka na nikasema nimemuona mke wangu. Na hivyo ndivyo nilipata mke wangu,” Njoya alieleza.

Jambo lingine la kushangaza ni kwamba askofu huyo alisimulia jinsi ‘alikufa na kufufuka’ siku tatu baadae akiwa hopsitalini.

Alisema kwamba kisa hicho kilimtokea mwaka 1989 wakati alikuwa anaongoza maandamao kupinga serikali ya hayati Daniel Moi wakati polisi walimshushia kipigo na mashambulizi ya kila rangi hadi kuzimia.

“Ilikuwa Jumamosi jioni wakati uongozi wa Moi ulituma polisi wakakuja kunishambulia, nawajua. Walinipiga na kunikatakata nikaachwa nimekufa. Walikuwa wengi, watu 9. Kabla ya kufa nikawaambia; ‘ndugu zangu kwa Bwana, mimi nimemsamehe na Mungu amemsamehe’, nikaenda. Siku ya tatu nikagutuka niko hospitali ya Nairobi, nilishangaa sana,” alisema.

“Nilikuwa nishaenda, niliona niko na Mungu mbinguni, nikafurahi sana. Nilikutana na Yesu, Malaika na watu wengi. Mbinguni ni furaha tu, haionekani na macho lakini inasikika. Malaika walikuwa wote ni Waafrika,” Njoya aliongeza.