Bensoul azungumzia jinsi kifo cha mamake kilimuathiri na alichojifunza kutokana nacho

"Kifo chake kwa kweli kiliathiri maisha yangu kwa njia nyingi sana na nahisi aliniacha jukumu hilo mikononi mwangu kwamba lazima niombee familia yangu, lazima niwashikilie niseme ni Yesu kwa maombi," alisema.

Muhtasari

• Msanii huyo alipata pia kuzungumzia alichojifunza kutoka kwa kifo cha mama yake, ambacho alikitangaza miezi minne iliyopita akiwa anatumbuiza jukwaani katika tamasha moja.

BVENSOUL
BVENSOUL
Image: facebook

Aliyekuwa msanii wa Sol Generation, Bensoul kwa mara ya kwanza amezungumzia jinsi kifo cha mamake miezi minne iliyopita.

Katika mazungumzo na SPM Buzz, Bensoul alisema kwamba kifo cha mamake kilikuwa pigo kubwa sana kwake kwake muda wote alikuwa ni mtu mtiifu kwa Mungu ambaye hangeanza siku kabla ya kuiweka familia yake mikononi mwa Mungu.

Msanii huyo alisema kwamba wakati mwingine anapoketi chini na kutafakari kuhusu maisha ya uchamungu aliyoishi mamake, anahisi kabisa kwamba ana jukumu la kuendeleza maisha hayo kwa vizazi vingine kiasi kwamba anatathmini kutunga nyimbo za injili.

“Mama yangu alikuwa ni yule mtu unaweza sema ni mkiristo kindakindaki, mwenye kila siku ya Mungu akirauka lazima aombe, huyo alikuwa ni mama yangu. Kifo chake kwa kweli kiliathiri maisha yangu kwa njia nyingi sana na nahisi aliniacha jukumu hilo mikononi mwangu kwamba lazima niombee familia yangu, lazima niwashikilie niseme ni Yesu kwa maombi, kwa hiyo tarajia nyimbo nyingi za injili kutoka kwangu,” Bensoul alisema.

Kuhusu kama kifo cha mamake kilifungua Baraka zake kwa kufanya vizuri kwa albamu yake ya Lion of Sudah, Bensoul alisema kwamba hawezi sema hivyo kwani bado anahisi kuna pengo kubwa lililosalia katika maisha yake na familia yao kwa jumla.

Msanii huyo alipata pia kuzungumzia alichojifunza kutoka kwa kifo cha mama yake, ambacho alikitangaza miezi minne iliyopita akiwa anatumbuiza jukwaani katika tamasha moja.

“Sidhani kama kifo chake kilikuwa Baraka kwa sababu nahisi kabisa kwamba aliacha pengo kubwa katika nyoyo zetu na  nafikiri ni funzo pia kwamba tunafaa kujumuika na watu wetu wakati wako hai katika njia mbalimbali.”

“Na pia mimi ninamsherehekea mamangu mara nyingi kwa sababu kama kuna mtu ambaye amenifunza mengi, ni yeye kwa sababu alikuwepo katika maisha yangu muda wote kama mfano mkubwa. Alinifunza kwamba ukienda huku utapotea, ukifuata njia hii utakuwa sawa…bila huo ushauri hamngekuwa na Bensoul sasa hivi,” Bensoul alisema.

“Pia kitu kingine nilichojifunza kutoka kumpoteza mamangu ni kwamba, watu wanaokuthamini wape maua yao wangali hai, kuwa karibu nao, hakikisha unaelewa ni nini walikuwa wanataka katika maisha yao, kama unaweza fanikisha kifanyike kwao, fanya, na kama huwezi, endelea kuwapa moyo kwamba siku moja kitatimia, kwa sababu kusema kweli hatutaishi hapa duniani milele,” aliongeza.