Israel Mbonyi: Mwimbaji maarufu wa ‘Nina Siri’ athibitisha kutumbuiza nchini Kenya mwezi Agosti

“Kenya ina nafasi muhimu katika nafsi yangu, na ninashukuru sana kwa upendo wenu usio na mipaka. Wakenya mmekuwa mashabiki wa kazi yangu ya muziki nambari moja katika kipindi cha miaka 3 iliyopita."

Muhtasari

• “Kwa muda mrefu imekuwa ni ndoto yangu kuja nchini Kenya na mwishowe ninakuja, alikeni rafiki zenu, familia ndugu jamaa na marafiki, Mungu awabariki,” alimaliza.

ISRAEL MBONYI
ISRAEL MBONYI
Image: Facebook

Mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za injili kutoka Rwanda, Israel Mbonyi hatimaye amethibitisha kwamba atakuwa nchini Kenya kwa ajili ya kutumbuiza kwa vibao vyake pendwa mwezi Agosti.

Mtunzi huyo maarufu kwa wimbo wake ‘Nina Siri’ ambao ni wimbo pendwa na idadi kubwa ya Wakenya alifichua taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa Instagram, akieleza furaha yake hatimaye kufika nchini Kenya kwa mara ya kwanza tangu kuvuma kwa nyimbo zake za injili.

“Habari zenu watu wazuri wa Kenya, mimi ni Israel Mbonyi na nina habari njema kuwataarifu, nina furaha kutangaza kwamba nitakuja nchini Kenya huu mwaka 2024. Nitakuwa natumbuiza moja kwa moja jijini Nairobi kwenye tamasha la Africa Worship Experience ugani Ulinzi Sports Complex mnamo Agosti 10,” Mbonyi alieleza.

Mtunzi huyo kutoka Rwanda pia alitambua jinsi Wakenya wamechangia katika kuenea kwa nyimbo zake, akisema kuwa wao ndio wamekuwa katika mstari wa mbele kuzipokea nyimbo zake kwa mikono miwili na kuzipenda.

“Kenya ina nafasi muhimu katika nafsi yangu, na ninashukuru sana kwa upendo wenu usio na mipaka. Wakenya mmekuwa mashabiki wa kazi yangu ya muziki nambari moja katika kipindi cha miaka 3 iliyopita na ninashukuru sana kwa hilo,” aliongeza.

Mbonyi aliweka wazi kwamba kwa muda mrefu imekuwa ndoto yake kuja nchini Kenya ili kujumuika na mashabiki wake katika kumtukuza Mungu kwa nyimbo zake pendwa, moja kwa moja.

“Kwa muda mrefu imekuwa ni ndoto yangu kuja nchini Kenya na mwishowe ninakuja, alikeni rafiki zenu, familia ndugu jamaa na marafiki, Mungu awabariki,” alimaliza.

Mbonyi alifunguka taarifa hizi, siku kadhaa baada ya kuwepo na uvumi kuhusu ujio wake.

Wiki mbili zilizopita, Mbonyi alichapisha picha yake akiwa na gitaa na kuuliza swali la balagha kuhusu ujio wake kenya, jambo lililowaacha mashabiki wengi na furaha na kumkaribisha.