CMB Prezzo atoa update kuhusu afya yake baada ya tukio la kuanguka akitumbuiza jukwaani

Wakati wa hafla ya uzinduzi wa kipindi cha uhalisia kwenye Netflix cha familia ya Bahati na Diana, Prezzo akiwa jukwaani kuwatumbuiza wageni alianguka katika tukio la kutia wasiwasi kwa mashabiki wake.

Muhtasari

• Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Prezzo amefichua kwamba yuko sawa na kufutilia mbali madai yanayoenezwa mitandaoni kuhusu tukio hilo la kuogopesha.

• Pia msanii huyo aliwashukuru wote waliofuatilia tukio hio baadae kwa kumpigia simu na kumuandikia jumbe za kutaka kujua hali yake inavyoendelea baada ya tukio hio.

Prezzo
Prezzo

Jackson Ngechu Makini maarufu kama CMB Prezzo, rapa wa muda mrefu humu nchini ametoa sasisho kuhusu afya yake saa chache baada ya tukio la kushtua la kuanguka akitumbuiza jukwaani.

Prezzo alikuwa miongoni mwa watumbuizaji walioalikwa kupamba na kufurahisha wageni katika hafla ya uzinduzi wa kipindi cha uhalisia cha familia ya msanii Bahati na Mkewe kitakachopeperushwa kwenye jukwaa la famu la Netflix.

Akiwa jukwaani, Prezzo alionekana kuanguka chini katika kile kilichotajwa kuwa ni kuzirai kwa ghafla, jambo ambalo liligeuza hafla hiyo kutoka kuwa ya furaha na kuwa ya kuhofia maisha ya msanii huyo mkongwe.

Hata hivyo, kupitia ukurasa wake wa Instagram, Prezzo amefichua kwamba yuko sawa na kufutilia mbali madai yanayoenezwa mitandaoni kuhusu tukio hilo la kuogopesha.

Prezzo alifichua kwamba katika siku za hivi karibuni, amekuwa akifanyisha mwili wake kazi nyingi sana na pengine ndicho kilichochangia mchoko uliopelekea yeye kuanguka, na kusema kwamba atalazimika kujitenga mbali kidogo na shughuli nyingi ili kutumia muda wake na familia yake.

“Kinyume na habari zinazoenezwa mitandaoni kuhusu afy yangu na tukio lililotokea jukwaani usiku wa juzi, ningependa kujulisha kila mmoja kwamba niko sawa. Unajua si rahisi kuwa mimi, nimekuwa nikifanya kazi nyingi siku za hivi karibuni, hivyo kupelekea mwili kuchoka,” alisema.

Pia msanii huyo aliwashukuru wote waliofuatilia tukio hio baadae kwa kumpigia simu na kumuandikia jumbe za kutaka kujua hali yake inavyoendelea baada ya tukio hio.

“Nawashukuru nyote kwa simu zenu na jumbe za kunitakia nafuu ya haraka. Ila kwa sasa ningependa kuchukua muda wangu mbali na kila kitu ili nitumikie kukaa karibu na familia yangu,” aliongeza.