Shorn Arwa awapa shavu wanandoa wenye ujasiri wa kuondoka ndoani mambo yanapopinda

Kwa mujibu wa Arwa, inauma sana kuona wanandoa wachanga kufikia uamuzi wa kuvunja ndoa zao chini ya miaka 5 baada ya kupendana, lakini akasema kwa upande mwingine ni uamuzi wa kijasiri kwa ajili ya afya ya kiakili.

Muhtasari

• “Moyo wangu unaenda nje kwa wanandoa wote wanaopitia changamoto hizi. Nawatumia upendo na sapoti yangu yote,” aliongeza.

• Katika kipindi cha miezi minne iliyopita, wanandoa wengi maarufu nchini wametangaza kusitisha penzi lao na kuwaacha mashabiki wa ndoa zao kwenye njia panda.

 

SHORN ARWA.
SHORN ARWA.
Image: INSTAGRAM

Mwanamitindo Shorn Arwa ametoa tamko lake kuhusu wimbi la wanandoa wachanga kuachana ambalo limeshamiri katika wiki ya kwanza ya mwezi huu wa Septemba.

Kupitia Instagtram, Arwa alitilia kwenye mizani suala hilo, saa chache baada ya Thee Pluto kufichua kuachana na Felicity Shiru, wiki moja baada ya Marya Okoth kutibitisha pia kuvunjika kwa ndoa yake na mchekeshaji YY.

Kwa mujibu wa Arwa, inauma sana kuona wanandoa wachanga kufikia uamuzi wa kuvunja ndoa zao chini ya miaka 5 baada ya kupendana, lakini akasema kwa upande mwingine ni uamuzi wa kijasiri kwa ajili ya afya ya kiakili.

“Hamjambo, nimekuwa nikifikiria sana kuhusu ndoa za watu wachanga siku za hivi majuzi. Ni vibaya sana kuona ndoa nyingi zao zikisambaratika, kwa kweli, inauma sana. Lakini kwa upande mwingine, ni jambo la kupendeza kuona kizazi hiki kimefunguka macho kiasi kwamba wana ujasiri wa kuweka kipaumbele suala la afya zao na kuondoka wakati mambo yanapokataa kuenda sawa,” Arwa alisema.

Arwa aliutoa moyo wake kwa wanandoa wote wachanga ambao wanang’ang’ana kuona kila siku wanasalia katika ndoa zao licha ya changamoto kibao.

“Moyo wangu unaenda nje kwa wanandoa wote wanaopitia changamoto hizi. Nawatumia upendo na sapoti yangu yote,” aliongeza.

Katika kipindi cha miezi minne iliyopita, wanandoa wengi maarufu nchini wametangaza kusitisha penzi lao na kuwaacha mashabiki wa ndoa zao kwenye njia panda.

Wimbi la kuachana lilianza mwezi Mei Khalif Khairo na Cera Imani walipotangaza kuachana wakifuatiwa na Teleh Pacbro na Martina huku mwezi Juni Kagwe Mungai na Sharon Mwangi wakiachana.

Julai Chris Kaiga na Joana Kinuthia walitangaza kuachana na Agosti ikawa zamu ya Size 8 na Dj Mo.