"Jiji langu!" Konshens ashindwa kujizuia kupitia Nairobi kabla ya kutumbuiza nchini Uganda

Konshens alifichua kuwa hataenda Uganda moja kwa moja lakini badala yake atapitia mji mkuu wa Kenya, Nairobi

Muhtasari

•Siku ya Jumanne usiku, mwanamuziki huyo tajika mwenye umri wa miaka 38 alichapisha picha iliyomuonyesha akiwa ndani ya ndege.

•Mapema mwezi huu, alitangaza kwamba angepitia nchini Kenya wakati wa safari yake ya muziki nchini Uganda kabla ya Krismasi.

Konshens
Image: HISANI

Msanii mashuhuri wa Dancehall kutoka Jamaica, Garfield Delano Spence almaarufu Konshens amedokeza kuwa atalala nchini Kenya mnamo usiku wa Jumatano, Desemba 13.

Siku ya Jumanne usiku, mwanamuziki huyo tajika mwenye umri wa miaka 38 alichapisha picha iliyomuonyesha akiwa ndani ya ndege.

Katika sehemu ya maelezo ya chapisho hilo, alifichua kuwa alikuwa njiani kuelekea nchi jirani ya Uganda ambako amepangwa kutumbuiza Jumapili, Desemba 17. Hata hivyo alifichua kuwa hatatua nchini Uganda moja kwa moja lakini badala yake atapitia mji mkuu wa Kenya, Nairobi

“Niko njiani kuelekea Uganda!! Nitawaona hivi karibuni!! Lakini nitalala Nairobi... ni nini motomoto Jumatano usiku katika jiji langu?” Konshens aliandika kwenye Twitter.

Mapema mwezi huu, staa huyo maarufu wa dancehall alitangaza kwamba angepitia nchini Kenya wakati wa safari yake ya muziki nchini Uganda kabla ya Krismasi.

Wakati alipokuwa akitoa tangazo hilo mnamo Desemba 5, Konshens aliwataka mashabiki wake kupendekeza maeneo mazuri ya kutembelea.

"Kwa taarifa yako, hakuna jinsi ninavyokuja Uganda niipendayo na nikose kupitia Kenya niipendayo hata ikiwa ni kwa vibes za likizo tu,, pendekeza maeneo kadhaa," alisema kupitia Twitter.

Haijabainika ikiwa mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 38 ana hafla iliyopangwa nchini Kenya au yuko hapa kwa likizo. Bado kuna siku tano zimesalia kabla ya onyesho lake la Uganda.

Sio mara ya kwanza kwa Konshens kuzuru Kenya. Ziara zake nyingi za awali hata hivyo zimekuwa safari za muziki ambapo ametoa maonyesho ya kusisimua.

Upendo mkubwa wa mwimbaji huyo wa Dancehall na Reggea kwa Kenya pia ni dhahiri shahiri na amethibitisha hilo kwa ziara zake kadhaa. Konshens ni mgeni wa mara kwa mara nchini Kenya na ziara yake ya mwisho ilikuwa Desemba 2021.

Wakenya wengi pia wanamshabikia Mjamaica huyo na hata kumfuatilia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Mapema mwaka huu, mwanamuziki huyo mahiri wa Dancehall alikiri kukubali jina la majazi ambalo alibandikwa na Wakenya kufuatia uhusiano na upendo wake mkubwa kwa taifa hili.

Upendo mkubwa wa mwimbaji huyo kwa Kenya uliwafanya watumiaji wa mitandao ya kijamii wabunifu kumpa jina Konshens Otieno na Mkenya mmoja hata akamtengenezea kitambulisho cha Kenya.

Konshens kwenye remix yake na rapa Boutross Munene ya wimbo maarufu 'Anjella' alionekana kulikubali jina hilo kwa moyo mkunjufu.

"Brace  pan di wall and fling it up gimmi nuh,

Konshens AKA Otieno,

Play with the two ni++le like Piano," Konshens aliimba.

Kwenye kitambulisho alichotengenezewa na Mkenya mbunifu, msanii huyo mzaliwa wa Jamaika alisemekana kuzaliwa Kisumu, Kenya.