Kabla sijawalipia karo watoto wangu wengine, huwa namlipia Morgan- Bahati akiri

Alifichua kuwa Morgan ana kisa cha kuhuzunisha sana na hivyo kuwataka Wakenya kuepuka kumshambulia.

Muhtasari

•Bahati alifichua kuwa yeye humpa Morgan upendeleo sana hadi humlipia karo ya shule kabla hata hajawalipia watoto wake wengine.

•Alifichua kuwa Morgan ana kisa cha kuhuzunisha sana na hivyo kuwataka Wakenya kuepuka kumshambulia.

Bahati na mwanawe Morgan
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Kelvin Kioko almaarufu Bahati amefunguka kuhusu upendo wake mkubwa  kwa mwanawe wa kulea Morgan Bahati.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na mchekeshaji Chipukeezy kwenye Chipukeezy Show, mwimbaji huyo alimtaja mvulana huyo wa miaka 13 kama mtoto maalum.

Alifichua kwamba yeye humpa Morgan upendeleo sana hadi humlipia karo ya shule kabla hata hajawalipia watoto wake wengine.

"Kabla ata nilipie watoto wengine wangu karo huwa nalipia Morgan," Bahati alisema.

Aliongeza, “Huwa naishi naye. Unajua watu wengi mitandaoni wameanza kutufuatilia baada ya Diana. Huyu ni mtoto nimekuwa naye hata kabla niingie kwa ndoa. Kwa hakika, wanawake wengi walinikataa kwa sababu ya mtoto huyu kwa sababu hakuna ambaye alikuwa kukaa na mtoto si wake.”

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili pia alitumia fursa hiyo kuwasihi wanamitandao na wanablogu kuwa na utu wakati wa kuandika hadithi zinazomhusisha mwanawe huyo.

Alifichua kuwa Morgan ana kisa cha kuhuzunisha sana na hivyo kuwataka Wakenya kuepuka kumshambulia wakati wanapokuwa wakishambulia familia yake.

"Sina shida na mtu yeyote kushambulia familia yangu, watoto wangu. Lakini usiwe unamshambulia mtoto wangu wa kwanza, Morgan. Nilimchukua mvulana huyu wakati wa msimu mgumu sana wa maisha yangu. Huyu ni mtoto nilimtoa kwa children’s home.

“Ako na hadithi ngumu sana ambayo sipendi kuirudia. Nilimchukua kutoka  nyumba ya watoto ambayo nilikuwa Mathare. Kabla hata aletwe kwa Children’s Home, ana hadithi ya kuhuzunisha sana. Kwa hiyo, hata kama nyie mnaandika kwa ajili ya kupata likes na views, tuwe na utu. Hawa ni watoto maalum," alisema.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Bahati aliandika barua ndefu kwa Morgan, siku chache tu baada ya mashambulizi ya mtandaoni.

Katika barua hiyo, alimhakikishia Morgan kuwa yeye ndiye baba yake licha ya mambo yote hasi yaliyosemwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kuthibitisha kujitolea kwake na upendo wake kwa mvulana huyo, Bahati alichukua fursa hiyo kusimulia safari ndefu ambayo wametembea pamoja tangu amchukue kutoka kwa nyumba ya watoto takriban miaka kumi iliyopita.

"Nimeitazama picha hii na nikagundua kuwa unakuwa Mwanaume. Hii ni miaka 10 iliyopita, siku ya kwanza nilipokutana nawe. Siku hiyo nilipoalika ABC Children's Home (ambapo nilikulia) kuja na kutumbuiza katika Uzinduzi wa Albamu yangu mwaka wa 2013 katika NPC Valley Road. Mwana nakumbuka siku ile kama Jana; jinsi ulivyolia na kuniita baba. Ilikuwa ngumu sana kwangu kuona wewe ukiwa na miaka 2 ukilazimisha kuingia kwenye basi linalorudi kwenye kituo cha watoto yatima; Niliona uchungu wako na nikajiona kupitia kwako; Kwa kuwa nimekua katika Nyumba ya Watoto wakati fulani, nikiwa pweke bila mtu wa Kumwita Mama au Baba!,” Bahati alisimulia chini ya picha zilizoonyesha ukuaji wa Morgan tangu walipokutana kwa mara ya kwanza hadi sasa.

Akaendelea, ” Mwanangu tangu siku ile; ingawa sikuwa tayari niliamua kuwa baba na nikakuchukua kama mwanangu. Mwana Nisikilize! Mimi ni Baba yako na Wewe ni Mwanangu! Mungu Alipanga Hakuna Kitu Kinachoweza Kubadili Hilo! Unapokua utaona mambo mengi ya Upuuzi na ya kinyama yanayosemwa kwenye Ulimwengu huu usio na huruma lakini kila wakati kumbuka licha ya yote, MIMI NI BABA YAKO NA WEWE NI MWANANGU! Mungu pekee ndiye Ajuaye yale tuliyopitia.”

Bahati pia alimhakikishia mwanawe kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kuahidi kumuunga mkono ili kufikia ndoto zake zote.