Karen Nyamu afunguka kuhusu kumpoteza mamake kutokana na saratani, kulelewa kanisani

Seneta Nyamu amefunguka kwa hisia kuhusu kifo cha mama yake miaka kadhaa iliyopita.

Muhtasari

•Nyamu alisema alikabiliana na kifo cha mama yake kwa kutokubali ukweli, jambo ambalo ameendelea kufanya hadi sasa

•“Bado nimeokoka, nampenda Mungu. Mtu hawezi kufika nilipo bila msingi wa neno la Mungu," seneta Nyamu alisema.

KAREN NYAMU
Image: FACEBOOK

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amefunguka kwa hisia kuhusu kifo cha mama yake miaka kadhaa iliyopita.

Katika mahojiano na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume Na Ene, wakili huyo alifichua kwamba mamake alikufa kutokana na ugonjwa hatari wa saratani wakati yeye alikuwa na umri wa miaka kumi na saba.

Nyamu alisema ilichukua muda kabla yeye na ndugu zake kujua ugonjwa aliokuwa anaugua mama yao kwani baba yao alijaribu sana kuwaficha ukweli.

"Alikuwa na saratani. Baba yangu alituficha sana habari hizo. Hata alipokuwa mgonjwa, hatukujua ni nini kibaya. Lakini alipoona mambo hayaendi sawa, alituita na kutuambia,” Karen Nyamu alisimulia.

Alifichua kuwa ni wakati ambapo marehemu mama yake alikuwa amelazwa hospitalini ambapo alijenga uhusiano wa karibu sana naye kabla yake hatimaye kufariki.

"Sikuwa kupata fursa ya kukua kutoka hatua ya kubalehe na kuwa na ukaribu sana na mama yangu," alisema.

Seneta huyo wa chama tawala cha UDA alisema alikabiliana na kifo cha mama yake kwa kutokubali ukweli, jambo ambalo ameendelea kufanya hadi sasa.

Alidokeza kuwa hajawahi kupona kabisa kutokana na msiba huo kwani huwa anajikuta akilia kila anapomkumbuka.

“Hata leo, kwa sababu nikimkumbuka nahisi kulia, huwa naondoa mawazo hayo. Siwezi kusema kuwa nimepona kwani sijawahi kukubali kusonga mbele,” alisema.

Katika mahojiano hayo, mama huyo wa watoto watatu pia alifichua kwamba alikulia katika familia ya Kikristo iliyoongozwa na maadili makali.

Alifichua kwamba wazazi wake na ndugu zake wanne walikuwa wameokoka na watu wanaokwenda kanisani, jambo lililomfanya kuwa mtoto mwenye nidhamu.

"Sijawahi kuwa mtukutu sana. Sikuwa na ushirika mbaya. Nilikuwa mtu wa kanisa kwa sababu tumelelewa kanisani. Hata marafiki niliowajua walikuwa washiriki wa brigedi, washiriki wa kundi la vijana wa kanisa na vikundi vya densi vya kanisa,” alisema.

Aliongeza, “Bado nimeokoka, nampenda Mungu. Mtu hawezi kufika nilipo bila msingi wa neno la Mungu.”

Bi Nyamu pia aliweka wazi kuwa tangu ujana wake alitaka kuwa wakili na akafichua alitaka kuwa kama kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua ambaye anasema alimuona kama kielelezo.