Khaligraph aomba Bien asipelekwe UK baada ya msanii wa Nigeria kukatalia huko alipopelekwa kutumbuiza

Baddo alipelekwa Uingereza kwa ajili ya shoo na baada ya onyesho alikimbia.

Muhtasari

•Kulingana na Khaligraph, Bien atakataa kurudi nchini Kenya iwapo atapata fursa nyingine ya kusafiri hadi jijini London.

• Baddo anasemekana kukimbia baada ya kutumbuiza na baadaye alimtumia promota ujumbe kupitia WhatsApp akimjulisha kuwa hajisikii kama Nigeria ni nyumbani.

Khalighaph Jones, Small Baddo, Bien
Image: INSTAGRAM

Rapa mashuhuri wa Kenya Khaligraph Jones amewasihi kwa utani mapromota wa muziki kutompeleka mwimbaji mwenzake Bien-Aime Baraza nchini Uingereza kutumbuiza katika matamasha.

Kulingana na rapa huyo mzaliwa wa mtaa wa Kayole, Bien angekataa kurudi nchini Kenya iwapo atapata fursa nyingine ya kusafiri hadi jijini London.

"Tafadhali usimpeleke tena @bienamiesol London, Hatarudi," Khaligraph aliomba kupitia mtandao wa Instagram.

Muimbaji huyo wa kibao ‘Yes Bana’ alitoa ombi hilo dhidi ya mshiriki mwenzake katika wimbo huo kufuatia taarifa za msanii chipukizi wa Nigeria Small Bado ambaye alidaiwa kukataa kurejea nchini kwao baada ya kupelekwa Uingereza kutumbuiza kwenye tamasha.

Katika jibu lake, Bien alibainisha kuwa London ni kama nyumbani kwake kwani kulingana naye, ni nyumbani kwa mkewe Chiki Kuruka.

“Ngombe wewe. London ni kwa akina @chikikuruka huko ni ushago kwetu na wife. Wewe Bwana Kayole ndio wanafaa kunyima Visa,” Bien alijibu.

Khaligraph alimjibu, “Usilie bro, Lakini London huendi tena. Nimeshakwambia.”

Kwa mujibu wa habari zilizosambaa, Baddo inasemekana alikimbia baada ya kutumbuiza na baadaye alimtumia promota huyo ujumbe kupitia mtandao wa WhatsApp akimjulisha kuwa hajisikii kama Nigeria ni nyumbani. Tukio hilo linaripotiwa kutokea mwaka wa 2021.

“Msanii mdogo wa Nigeria, Small Baddo alipelekwa Uingereza kwa ajili ya shoo na promota wa hafla, na baada ya onyesho alikimbia. Msanii huyo mdogo alimwandikia promota wa hafla hiyo kwenye WhatsApp akimwambia hatarudi Nigeria kwa sababu "Nigeria sio yake!" ripoti ya Music Base Africa ilisema.

Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa promota huyo, Billyque B alitozwa faini ya pauni 60000 (Ksh 10.8milioni) kufuatia sakata hiyo kwani muda wa Visa ya Baddo ya Uingereza ulikuwa umeisha.

"Leseni ya promota kuleta Wasanii wengine nchini Uingereza inaweza kuchukuliwa ikiwa Small Baddoo hatatokea. Promota wa hafla hiyo tayari ametozwa faini ya £6000 kwa kuwa visa ya Small Baddo ya Uingereza imeisha muda wake,” ilisoma ripoti hiyo.

Billyque inasemekana aliomba msaada kutoka kwa watu kumsaidia kumtafuta msanii huyo mchanga ili kumrudisha Nigeria.