Sijawahi kukutana na baba yangu mzazi, asema Mammito

Kwa kiasi kikubwa anasema kuwa aliyemshika mkono hadi alipo sasa ni mama yake.

Muhtasari

•Mammito amezaliwa katika mazingira ya mama mlezi wa kipekee , tangu alipozaliwa Hajapata kumjua baba yake.

•“Mimi nililelewa na mama yangu pekee na hakuna chochote tulichokosa , sikuhisi kukosa baba kwa kuwa mama alihakikisha kuwa tuko na kila kitu tunachohitaji “ alisema.

mammito
Mchekeshaji Eunice Mammito mammito
Image: HISANI

Eunice Wanjiru Njoki kwa jina maarufu nchini Kenya Mammito , ni mmoja wa wanawake ambao wanatoa burudani ya kuchekesha Afrika mashariki.

Ikiwa mwaka huu amehitimisha miaka 30 yeye ni kielelezo chema hasa kwa kina dada ambao wana ndoto za kuingia kwenye tasnia ya vichekesho

Mbali na kuwa Mammito ni mchekeshaji maarufu , pia ni mtayarishaji wa maudhui akiwa ni miongoni mwa wachekeshaji ambao wanaongoza kutoka bara Afrika.

Ucheshi wake sambamba na mtindo wake wa maneno ni kivutio cha wengi .

Aidha mwanadada huyu anatumia matukio ya kila siku ya watu walio karibu na yeye na kutumia kwenye ucheshi wake .

"Kuishi na kujionea matukio mengi maishani ndio kumenipa mtindo wangu. Ndiyo maana kila nilipo ninapenda kutangamana na watu na mazingira ili pia nipate uzoefu mpya kila wakati ninapotumbuiza ” anasema Mammit

Malezi ya Mammito

Kwa kiasi kikubwa anasema kuwa aliyemshika mkono hadi alipo sasa ni mama yake hasa wakati alikuwa anakulia katika mmojawapo ya vitongoji vikubwa nchini Kenya huko Kibera .

“Mama yangu siku zote alipenda vichekesho na aliunga mkono dhamira yangu.” anasema Mammito .

Dada huyu alianza kutumbuiza kanisani , kuanzia wakati ana umri wa miaka , mitano. Baadaye alianza kutumbuiza na vikundi mbalimbali vya wasanii vikiwemo ‘Pillars of Kibera’ kikundi cha wasanii wa ngoma za asili ambapo alifanya sanaa mbalimbali.

Aidha anasema kuwa matukio mbalimbali ya kufanya sanaa akiwa mitaani yalimpa moyo kwa kuwa aliigiza na kuimba mashairi ya matukio mbalimbali wakati huo.

Mammito alizaliwa Jimbo la Nairobi. Yeye amezaliwa katika mazingira ya mama mlezi wa kipekee , tangu alipozaliwa Hajapata kumjua baba yake, na kila wakati amenukuliwa akisema kuwa hajui jinsi mtu anavyohisi kuwa na baba.

“Mimi nililelewa na mama yangu pekee na hakuna chochote tulichokosa , sikuhisi kukosa baba kwa kuwa mama alihakikisha kuwa tuko na kila kitu tunachohitaji “. Anasema Mammito.

Katika mazingira ya kulelewa kitongoji duni Kibera dada huyu anasema kuwa Kupata mlo pekee katika mitaa waliyoishi ilikuwa ni ngumu sana, kwasababu maisha huko yalikuwa na changamoto za aina yake, Mammito anasema kuwa mama yake alikuwa ni mlezi ambaye alihitaji wanae wafaulu na kwa hivyo alikuwa mkali kwenye masuala ya nidhamu na hakumruhusu kucheza na watoto wa jirani, wakiwa wadogo .

Kuingia kwenye tasnia ya uchekeshaji

Mapenzi ya Mammito kwenye vichekesho ulikuwa mpaka chuo kikuu, ambapo alitumbuiza katika maonesho ya vipaji. Mara nyingi aliwavutia waamuzi kwa kiasi kwamba aliibuka kushangiliwa na mwenye kupendwa na waliomfuatilia wakati huo .

Kutokana na hayo Mammito aliendelea kufanya majaribio nchini Kenya katika kipindi cha 'The Churchill Show' , alijaribu mara kadhaa akishindwa kupata nafasi ya kutumbuiza kwenye kipindi hicho . Anasema kuwa wakati huo alikuwa na hofu ya jukwaa na pia watu .

Licha ya hayo, hakukata tamaa ya kuwa angefua dafu katika fani ya uchekeshaji , aliendelea kufanya majaribio katika jukwaa hilo hadi alipofanikiwa.

Tangu alipopata nafasi ya kwanza ya kutumbuiza katika kipindi cha ‘Churchill Show’ ameibuka kuwa mmoja wa wachekeshaji walio bora nchini Kenya na hata nje ya nchi.

Mbali na kazi zake maarufu za kuwa mcheshi, Mammito ni mfanyabiashara.

Mammito amezuru nchi mbali mbali kwa ajili ya sanaa yake ya uchekeshaji ikiwemo Afrika Kusini , Botswana, Tanzania, Eswatini, Uganda, Sudan Kusini, Dubai na Rwanda.