Mbunge Jalang’o alazwa hospitalini baada ya kuugua jeraha

Jalang’o alipata jeraha kwenye mguu wake wa kushoto alipokuwa akicheza mpira wa vikapu.

Muhtasari

•Mtangazaji huyo wa zamani wa redio alishiriki video yake akiwa hospitalini ambako amelazwa katika wadi ya kibinafsi.

•Wakati akifichua habari kuhusu jeraha hilo siku ya Jumatano, aliitaja kama "jeraha la kwanza la msimu."

akifanyiwa uchunguzi wa MRI katika hospitali ya Nairobi.
Mbunge Jalang'o akifanyiwa uchunguzi wa MRI katika hospitali ya Nairobi.
Image: HISANI

Mbunge wa eneo la Lang’ata Phelix Odiwour anaendelea na matibabu baada ya kupata jeraha la mguu wa kushoto alipokuwa akicheza mpira wa vikapu mapema wiki hii.

Siku ya Alhamisi, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alishiriki video yake akiwa hospitalini ambako amelazwa katika wadi ya kibinafsi.

"Siku ya pili hapa, maisha ya hospitali," Jalang'o aliandika chini ya video aliyochapisha kwenye mtandao wa Instagram.

Katika video hiyo, mchekeshaji huyo alionekana akiwa amelala kitandani huku akishiriki mazungumzo na mhudumu wa hospitali anayemhudumia. Pia alionyesha mguu wake ambao ulijeruhiwa.

Jalang’o alipata jeraha kwenye mguu wake wa kushoto alipokuwa akicheza mchezo wake anaoupenda zaidi, mpira wa vikapu mnamo Septemba 27. Kisha alipelekwa katika Hospitali ya Nairobi ambako uchunguzi wa MRI ulifanyika.

Wakati akifichua habari kuhusu jeraha hilo kwenye video siku ya Jumatano, aliitaja kama "jeraha la kwanza la msimu."

Baada ya kupata jeraha hilo, kundi la watoa huduma ya kwanza walionekana wakishughulikia mguu wake uliojeruhiwa kabla ya kumshauri atembelee hospitali na kufanyiwa uchunguzi wa MRI mara moja.

“Nitaenda hospitali leo. Nimetengwa. Nitaenda kwa MRI," alisikika akisema. 

Baadaye alidokeza kuwa uchunguzi wa MRI ulibainisha jeraha lake lilihitaji matibabu maalum, jambo lililopelekea yeye kulazwa.

"Nilithani ni jeraha ndogo,.. natabasamu kwenye mashine ya MRI," alisema huku akionyesha akifanyiwa uchunguzi wa MRI.

Jeraha hilo limemlazimu mbunge huyo wa muhul wa kwanza kuchukua mapumziko kutoka mazoezini na timu ya mpira wa vikapu ya Bunge la Kitaifa.