Mmoja afariki katika ajali mbaya ya barabarani iliyomhusisha msanii wa Marioo (+video)

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kabuku Jumamosi ambapo waathiriwa kadhaa wanaripotiwa kupata majeraha mabaya.

Muhtasari

•Mtayarishaji wa muziki waTanzania Abbah Process alithibitisha kifo cha Nabeel Jumapili asubuhi alipokuwa akimuomboleza.

•Wengine wanaripotiwa kuvunjika miguu kufuatia ajali hiyo huku msanii Chino Kidd akisemekana kuumia zaidi kifuani.

Msanii Chino Kidd na marehemu Nabeel
Image: INSTAGRAM// ABBAH PROCESS

Mwanaume mmoja amefariki dunia kufuatia ajali mbaya iliyotoea siku ya Jumamosi ambayo ilimhusisha msanii wa Tanzania, Chino Kidd na kundi lake la muziki.

Chino Kidd ambaye anapendelea kuimba mtindo wa Amapiano  na wenzake kadhaa walikuwa wakielekea katika mkoa wa Tanga, Tanzania kwa ajili ya shoo wakati gari aina ya Alphard nyeusi walilokuwa wamepanda liligongana na lori la mafuta ya petroli.

Ajali hiyo inaripotiwa kutokea katika eneo la Kabuku Jumamosi mchana ambapo waathiriwa kadhaa wanaripotiwa kupata majeraha mabaya.

“Tulikuwa tunaelekea Tanga katika show ya mama yetu Ummy Mwalimu, ajali tumeipata maeneo ya Kabuku, tuliondoka na gari mbili, gari alilokuwa amepanda msanii likuwa limetangulia na msanii alikuwa amekaa upande wa kushoto wa dereva,” Meneja wa Chino Kidd, Sweder aliambia Tanzania Web.

Meneja huyo alisema waathiriwa walifanikiwa kupata usaidizi wa haraka baada ya ajali hiyo na majeruhi kukimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Tanga. Alisema kuwa wote waliokuwa kwenye gari hilo walipata majeraha lakini hakuna aliyefariki papo hapo.

Kwa bahati mbaya, dereva wa Alphard hiyo nyeusi iliyokuwa imembeba msanii Chino Kidd, aliyetambulika kwa jina la Nabeel ameripotiwa kufariki.

Mtayarishaji wa muziki kutoka Tanzania Abbah Process alithibitisha kifo cha Nabeel Jumapili asubuhi alipokuwa akimuomboleza.

“Rest in peace brother, tumepoteza mwanafamilia mmoja aliyekuwa kwenye ajali ya jana (Jumamosi). Mungu amkumbatie katika mikono yake yenye upendo na ampe amani ya milele. Milele mioyoni mwetu,” Abbah Process aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram.

Waathiriwa wengine wanaripotiwa kuvunjika miguu kufuatia ajali hiyo huku Chino Kidd akisemekana kuumia zaidi kifuani.

Video iliyoshirikiwa na producer Abbah inaonyesha watu wakiwa wamekusanyika karibu na Alphard nyeusi ambayo ilikuwa imembeba Chino na wenzake. Gari hilo linaonekana kugongwa vibaya haswa upande wa kulia. Lori la mafuta ya petroli ambalo pia lilihusika katika ajali hiyo likionekana upande wa pili wa barabara likiwa limeelekeza kichwa chini.

Chino Kidd ni mmoja wa wasanii waliosajiliwa chini ya lebo ya muziki ya Bad Nation inayomilikiwa na Marioo.