Mshambulizi Emmanuel Adebayor aonekana akijivinjari jijini Nairobi (+video)

Mchezaji huyo alifichua kwamba atakuwa humu nchini kwa kipindi cha wiki moja.

Muhtasari

•Adebayor alitua Kenya siku isiyothibitishwa na alionekana akijivinjari katika moja ya klabu kubwa jijini Nairobi.

•Kwa sasa Adebayor anachezea klabu ya Togo, Semassi baada ya kucheza Ulaya kwa takriban miongo miwili.

Image: INSTAGRAM// EMMANUEL ADEBAYOR

Mshambulizi wa zamani wa Arsenal, Tottenham na Manchester City Sheyi Emmanuel Adebayor yupo hapa nchini Kenya.

Adebayor alitua Kenya siku isiyothibitishwa na alionekana akijivinjari katika moja ya klabu kubwa jijini Nairobi.

Katika video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, mchezaji huyo wa kimataifa wa Togo alionekana akinengua kiuno na kushiriki vinywaji pamoja na watu wengine ambao walikuwa wameenda kujivinjari katika klabu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alifichua kwamba atakuwa humu nchini kwa kipindi cha wiki moja.

"Tunabarizi, kunapendeza. Napenda. Nitakuwa wiki moja," Adebayor alimwambia Nimrod Nick.

Kwa sasa Adebayor anachezea klabu ya Togo, Semassi baada ya kucheza Ulaya kwa takriban miongo miwili.

Mshambulizi huyo alianza taaluma yake ya soka katika klabu ya Metz nchini Ufaransa, kisha akachezea Monaco kabla ya kujiunga na Wanabunduki mwaka wa 2006. Alicheza katika Arsenal kwa takriban miaka mitatu kabla ya kujiunga na Manchester City.

Baadaye alichezea klabu nyingine kubwa za Ulaya kama vile Tottenham, Real Madrid, Crystal Palace, İstanbul Başakşehir na Kayserispor. Alimaliza safari yake ya ughaibuni nchini Paraguay ambapo alichezea Club Olimpia kabla ya kurejea nchi yake ya Togo ili kuichezea Semassi mwaka wa 2021.

Tazama video hapa:-▶▶▶