Mtangazaji wa Inooro TV, Ken Wakuraya akamatwa Kasarani

Ken alilalamika kwamba hakufahamu ni wapi yeye na wengine waliokamatwa naye walikuwa wakipelekwa.

Muhtasari

•Muigizaji huyo wa zamani wa Tahidi High alidai kuwa maafisa wa polisi walimkamata kwa sababu alikosa kulipa Ksh 20,000.

•Wengine pia walisikika wakilalamika kwamba maafisa hao walichukua simu zao.

Image: FACEBOOK// KEN WAKURAYA

Mtangazaji wa Inooro TV Ken Wakuraya alikamatwa siku ya Jumamosi jioni alipokuwa akitumbuiza katika klabu moja maarufu eneo la Kasarani, Nairobi.

Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook, muigizaji huyo wa zamani wa Tahidi High alidai kuwa maafisa wa polisi walimkamata kwa sababu alikosa kulipa Ksh 20,000.

Alilalamika kwamba hakufahamu ni wapi yeye na wengine waliokamatwa naye walikuwa wakipelekwa.

“Hii ni Kenya gani? Je, kuna amri ya kutotoka nje? Kwa nini kuwakamata wasanii. Nimekamatwa, sasa niko kwenye gari la polisi kwa sababu siwezi kulipa 20k. Sijui tunakoelekea," Ken aliandika Jumamosi jioni.

Mtangazaji huyo ambaye pia ni mtumbuizaji wa Muziki wa Country alishiriki video za moja kwa moja zilizowaonyesha wakiwa wamebebwa kwenye gari la polisi. Video hizo hazikuwa wazi vya kutosha kwani ilikuwa ni usiku sana.

Katika mojawapo ya video hizo, sauti zilisikika zikilalamika kuhusu kutendewa vibaya na maafisa hao. Wengine pia walisikika wakilalamika kwamba maafisa hao walichukua simu zao.

Katika video nyingine, watumbuizaji waliokamatwa walisikika wakipiga kelele na kusema kwa sauti, "wezi, wezi, wezi nyinyi!" huku wakigonga kuta za gari walilokuwemo.

“Sasa ni nani wengine wanapiga kelele? Sasa juu mmetushika kelele imepungua Nairobi,” mmoja wa waliokamatwa alisikika akilalamika.

Mwingine aliyekamatwa alisikika akilia kwa sauti kubwa akilalamika kwamba pingu alizowekwa mikononi zilikuwa zikichanika nyama yake.

“Inanikata mikono, fungueni mimi, nifungueni, nitakufa,” alisikika akilia kwa nguvu. 

Ken pia alionyesha pingu zilizokuwa mikononi mwake na kusema, "Hii ni mikono yangu. Wamenishika wakaniweka pingu. Mimi ni msanii. Nimeibia nani? Nilikuwa natumbuiza na nilikuwa moja kwa moja. Serikali inajua nilikuwa natumbuiza. Nimeiba wapi.”

Haijabainika iwapo mtangazaji huyo na wenzake wengine waliokamatwa walilala chini ya ulinzi wa polisi au waliachiliwa baadaye.

Kabla ya kukamatwa, Ken awali alikuwa ameshiriki video za moja kwa moja zake akiburudisha washereheshaji kwa muziki wa Country jukwaani.