"Ni mwanangu wa pekee!" Kajala amuonyesha upendo mkubwa mkwe wake Marioo

Kajala alimtambua Marioo kama mwanawe wa pekee na kufunguka kuhusu upendo wake kwake.

Muhtasari

•Muigizaji Kajala Masanja ameendelea kukiri upendo wake mkubwa kwa mwimbaji Omari Mwanga almaarufu Marioo. 

•Kajala alimtambua mwimbaji huyo kama mwanawe na akafichua kuwa wanafanya mipango mikubwa pamoja.

Paula Kajala, Marioo, Kajala Masanja
Image: HISANI

Muigizaji mkongwe wa filamu bongo Fridah Kajala Masanja ameendelea kukiri upendo wake mkubwa kwa mwimbaji Omari Mwanga almaarufu Marioo. 

Marioo kwa sasa anachumbiana na bintiye Kajala, Paula Paul mwenye umri wa miaka 21 na wawili hao wamekuwa wakijivunia kuonyesha mapenzi yao hadharani kwa miezi kadhaa iliyopita.  

Katika taarifa fupi kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatatu, mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa Kondegang Harmonize alimtambua Marioo kama mwanawe wa pekee na kufunguka kuhusu upendo wake kwake.

“Ni mwana pekee niliye naye ,@marioo_tz makopa mengi sana kwako,” Kajala aliandika na kuambatanisha na emoji za moyo zinazoashiria upendo.

Ujumbe wa Kajala uliandamana na picha ya mwimbaji huyo wa kibao 'Mi Amor'.

Siku ya Jumamosi jioni, Kajala alifanya karamu kubwa ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa ambapo Marioo alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa waliopamba hafla hiyo. Muigizaji huyo alisherehekea siku yake maalum kwa mtindo huku akitimiza miaka 40.

Marioo alitumia hafla hiyo kummiminia upendo mama mkwe wake na kumthamini kwa kumpa binti yake.

“Upendo ambao naupata kutoka kwa mama mkwe ni mkubwa sana. Tushaongea vitu vingi mimi na mama yangu, tumeshapanga vitu vingi sana. Mimi niseme tu nampenda sana na Mungu amfanyie upesi mambo yazidi kuwa mazuri,” Marioo alisema mbele ya wageni waliokuwa wamejumuika kwa karamu hiyo.

Aliongeza, “Nafurahi kwamba kanikabidhi mtoto, sio rasmi lakini. Nimefurahi, nashukuru nampenda sana mama yangu. Mungu akubariki.”

Baada ya hotuba yake, Marioo alifikia begi lililojaa pesa ambazo alikusudia kumpa mpenzi huyo wa zamani wa bosi wa Kondegang Harmonize kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Kabla ya kupokea pesa hizo, Kajala alifunguka kuhusu uhusiano mzuri kati yake na mkwe wake Marioo.

Alimtambua mwimbaji huyo kama mwanawe na akafichua kuwa wanafanya mipango mikubwa pamoja.

“Omari ni kijana wangu. Tuko poa sana, tunaingia vizuri mno. Tunaongea vitu vingi sana, ata asiponipa mimi chochote hapa, niko poa kwa sababu kuna vitu vingi sana tunafanya nyuma ya pazia nyinyi hata hamjui. Uwepo wake hapa ni mkubwa mnachotaka atoe kwenye sahani. Shukran kwa kuja,” Kajala alisema.

Baada ya kusifiwa, Marioo aliendelea kumuogesha mama huyo wa mpenzi wake noti za pesa kiasi ambacho hakikujulikana.