Nyota Ndogo ashangazwa na upendo mkubwa wa mama mkwe wake mzungu

“Naipenda. Ninahisi joto tayari. Ni nzuri. Asante sana. Naipenda.” Nyota Ndogo alimwambia mama mkwe wake.

Muhtasari

•Nyota Ndogo alichapisha video inayomuonyesha mama mkwe wake akimpa sweta ambayo alikuwa amemtengenezea ili asiteseke chini ya baridi kali katika nchi hiyo ya Ulaya.

•"Mimi mwenyewe huko nyuma nilikuwa najiuliza kweli nitakuja kupendwa kweli? Ila Mungu anatupangia safari yetu. Nikavumilia tu,” alisema Nyota Ndogo.

Nyota Ndogo na mama mkwewe
Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwimbaji mkongwe Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo amejigamba kuhusu mapenzi mazito ambayo amekuwa akipata kutoka kwa wakwe zake.

Siku ya Jumapili, mwimbaji huyo mzaliwa wa Pwani ambaye kwa sasa yuko ziarani kwa wakwe zake nchini Denmark alichapisha video inayomuonyesha mama mkwe wake akimpa sweta ambayo alikuwa amemtengenezea ili asiteseke chini ya hali ya hewa ya baridi kali katika nchi hiyo ya Ulaya.

Nyota Ndogo alifichua kuwa mama mkwe wake amekuwa akimwonyesha upendo mwingi tangu alipofika huko.

"Upendo wa mama. Mapenzi haya hayana masharti, ama nimekosea kizungu? Hii wiki yote amekuwa akinionyesha upendo. Mimi nawaambia nikifika huku huwa nafeel kama kamtoto kadogo. Nadekezwa na kila mtu,” Nyota Ndogo alisema chini ya video ambayo alichapisha kwenye mtandao wa Instagram.

Aliongeza, “Ni mapenzi kila mwanamke anastahili kuyapata. Maana mimi mwenyewe huko nyuma nilikuwa najiuliza kweli nitakuja kupendwa kweli? Ila Mungu anatupangia safari yetu. Nikavumilia tu.

Katika video hiyo, mama huyo wa watoto wawili alionekana kujawa na bashasha wakati akipokea sweta hiyo  iliyofumwa vizuri kutoka kwa mama mkwe wake.

“Hii ni kwa ajili yako. Nilikutengenezea mwaka jana. Nilisema utakuja kututembelea wakati wa baridi na Denmark kuna baridi sweta na sweta hii iko na joto. Unaweza kuivaa,” mama mkwe alimwambia mwimbaji huyo.

Huku akijibu, Nyota Ndogo ambaye hakuweza kuficha furaha usoni mwake alimwambia mama huyo wa mumewe Henning Neilsen, “Naipenda. Ninahisi joto tayari. Ni nzuri. Asante sana. Naipenda.”

Takriban wiki moja iliyopita, Nyota Ndogo alichapisha picha iliyomuonyesha akiwa na mumewe Henning Nielsen, wazazi wakwewe, kaka ya mumewe na mkewe.

Huku akitoa maelezo ya picha hiyo, Nyota Ndogo alifichua kuwa amekubaliwa vizuri na wakwe zake wa Uholanzi na wana uhusiano mzuri.

"Ukichukiwa na familia nzima lakini mumeo akupende hiyo inatosha. Lakini ikitokea unapendwa na familia nzima mpaka mumeo unajiskia furaha isiyo na kifani,"  Nyota Ndogo alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

"Hapo ni kaka wawili na wake zao, na wazazi wao.Picha ya familia," aliandika chini ya picha ambayo alichapisha.

Pichani, familia hiyo ilionekana kuwa na bashasha na kufurahiya kuwa pamoja. Wote walivalia tabasamu zuri kwenye nyuso zao.