Nyota Ndogo awatambulisha wakwe zake wazungu huku akifichua uhusiano wake mzuri nao

Nyota Ndogo alifichua kuwa amekubaliwa vizuri na wakwe zake wa Uholanzi na wana uhusiano mzuri.

Muhtasari

•Nyota Ndogo alichapisha picha iliyomuonyesha akiwa na mumewe Henning Nielsen, wazazi wakwewe, kaka ya mumewe na mkewe.

•Familia hiyo ilionekana kuwa na bashasha na kufurahiya kuwa pamoja. Wote walivalia tabasamu zuri kwenye nyuso zao.

Nyota Ndogo, mumewe na wakwe zake
Image: INSTAGRAM

Mwimbaji mzaliwa wa Pwani,  Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo amewatambulisha wakwe zake wazungu kwa mashabiki wake.

Siku ya Ijumaa, mama huyo wa watoto wawili alichapisha picha iliyomuonyesha akiwa na mumewe Henning Nielsen, wazazi wakwewe, kaka ya mumewe na mkewe.

Huku akitoa maelezo ya picha hiyo, Nyota Ndogo alifichua kuwa amekubaliwa vizuri na wakwe zake wa Uholanzi na wana uhusiano mzuri.

"Ukichukiwa na familia nzima lakini mumeo akupende hiyo inatosha. Lakini ikitokea unapendwa na familia nzima mpaka mumeo unajiskia furaha isiyo na kifani,"  Nyota Ndogo alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

"Hapo ni kaka wawili na wake zao, na wazazi wao.Picha ya familia," aliandika chini ya picha ambayo alichapisha.

Pichani, familia hiyo ilionekana kuwa na bashasha na kufurahiya kuwa pamoja. Wote walivalia tabasamu zuri kwenye nyuso zao.

Nyota Ndogo kwa sasa yuko na mumewe nchini Uholanzi na wawili hao wamekuwa wakifurahia wakati pamoja.

Siku ya Alhamisi, mwimbaji huyo mkongwe alionyesha akishiriki muda akiwa na mke wa zamani wa mumewe na mume wake mpya pia.

Uhusiano wao mzuri ulimpendeza Nyota Ndogo ambaye aliandika kuhusu ukosefu wa wivu ambao uliwafanya wenzi wa zamani bado kutumia wakati pamoja.

"Nimejifunza mambo mengi kwa wazungu but nilichopenda zaidi nikua hawa watu wakiachana na waliwahi kuzaa huwa familia inaendeleza upendo hata ya kirafiki.Ukimuangalia aliposimama mume wangu, yaAni hio team huyu mama ni aliyekuwa mke wake kisha huyu mschana ni mtoto wao na mjukuu so wapo team moja upande wa pili tupo team na dada zake na mume wake wa saa hizi.

Yaani hakuna chuki yaani ikifika birthday ya watoto wao ama wajukuu familia zote zinakuja mume wangu na mimi na aliekua mke wake nae anakuja na mume wake. Huyu mama waliachana kitambo sana hata sijajua ntakua kwenye picha na uko alikoolewa yupo na wasichana wameolewa pia," alieleza.

Mwaka jana, mwanamuziki huyo alifunguka kuhusu upendo mkubwa ambao wazazi wa mumewe wamemuonyesha tangu alipojiunga na familia.

"Hii familia imenipokea kwa mikono miwili, ina mapenzi mengi sana kwangu. Nafurahi sana kuwa mmoja wa familia hii," alisema.

Nyota Ndogo na Bw Henning Nielsen wamekuwa kwenye ndoa ya mbali kwa takriban miaka sita. Wanandoa hao wawili walifunga pingu za maisha mwezi Mei 2016 baada ya kuchumbiana kwa muda.

Mapema mwaka huu Nyota Ndogo alifichua kuwa  ilichukua mwaka mmoja kwa yeye kujibu ombi la ndoa la mumewe huyo mzungu.