"Tutamzika kama mwanajeshi" Eric Omondi amuomboleza Baby Payden kwa uchungu

"Alipigana vita vizuri. Alikimbia mbio zake. Katika muda mfupi alioishi, alinifundisha masomo makubwa," Eric Omondi aliomboleza.

Muhtasari

•Eric ambaye alikuwa amejitolea kusaidia katika safari ya matibabu Payden alimuomboleza kama mtoto mwenye nguvu.

•Eric aliwahamasisha Wakenya kuchanga zaidi ya Ksh 600,000 kwa ajili ya mtoto huyo mgonjwa ambaye sasa kwa bahati mbaya amepoteza maisha yake.

akiwa amemshika mtoto Payden Mudoga huku mamake akitazama.
Eric Omondi akiwa amemshika mtoto Payden Mudoga huku mamake akitazama.
Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji Eric Omondi amethibitisha kifo cha mtoto wa mwezi mmoja, Payden Mudoga ambaye alikuwa na uvimbe wa saratani kwenye taya.

Wakati akitangaza kifo cha Payden siku ya Jumatatu asubuhi, Eric ambaye alikuwa amejitolea kusaidia katika safari ya matibabu ya mvulana huyo mchanga alimuomboleza kama mtoto mwenye nguvu kuweka wazi kuwa marehemu alipigania afya yake vyema.

“Tumempoteza mtoto Payden. Payden alikuwa Mtoto mwenye Nguvu sana. Alipigana vita vizuri. Alikimbia mbio zake. Katika muda mfupi alioishi, alinifundisha masomo makubwa. Alifundisha Ustahimilivu. Amepumzika. Tutamkumbuka kama Legendari,” Eric Omondi alitangaza kupitia mtandao wa Instagram.

Aliongeza, “Tutasherehekea maisha yake. Tutamzika kama Mwana wa Mfalme. Mungu ampe pumziko. Hatutapoteza matumaini, tutamzika kama mwanajeshi tukiwa tumeinua vichwa vyetu juu. Kwa mara nyingine tena, Asanteni kwa WOTE Mliochangia. Tutaendelea.

Kifo cha Payden kinakuja siku chache tu baada ya mchekeshaji huyo maarufu kupanga uhamisho wake kutoka hospitali alimokuwa amelazwa hadi katika kituo cha matibabu cha hali ya juu baada ya kuwaleta Wakenya pamoja ili kuchangia fedha za matibabu yake.

Wiki iliyopita, Eric alikuwa amefichua tatizo la kiafya la mvulana huyo mchanga na kuwahamasisha Wakenya kuchangia matibabu yake kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

“Huyu ni mtoto Pyden Mudoga, ana mwezi mmoja tu. Nimemtembelea mara kadhaa hospitalini na kila ninapomkuta analia, ana uvimbe wa saratani kwenye Taya na anaumwa kila mara. LAZIMA TUKOMESHE maumivu,” Eric alifichua wiki jana.

Aliambatanisha kauli yake na video iliyomuonyesha akiwa amemshika Payden ambaye wakati huo alikuwa akilia sana bila kujizuia huku mama yake akimtazama tu kwa uchungu.

“Huyu ni mama yake, Magdalene Khamisi, mwanamke mwenye nguvu sana. Leo usiku kuanzia saa mbili jioni hadi saa sita usiku nitakuwa nikichangisha pesa kwa ajili ya mtoto na mama kwenye akaunti zangu zote za mitandao ya kijamii. ANZA KUTUMA PESA kwa namba ya mama 0757845548 (Jina: MAGDALENE KHAMISI). Tuchange za kutosha kumtibu mtoto na kusaidia familia kuhama kutoka katika chumba chao kimoja katika mtaa wa Kawangware hadi nyumba bora,” aliongeza.

Baadaye jioni hiyo, mchekeshaji huyo alifanikiwa kuwahamasisha Wakenya kuchangisha zaidi ya Ksh 600,000 kwa ajili ya mtoto huyo mgonjwa ambaye sasa kwa bahati mbaya amepoteza maisha yake.