Wakati wa kihisia huku Nanny Rosie akirejea Lebanon licha ya mwajiri wake kutaka asirudi (+video)

Rosie amekuwa nchini Kenya na familia yake kwa chini ya miezi miwili tu.

Muhtasari

•Rosie alikaribishwa kwenye uwanja wa ndege na mwajiri wake na watoto wake wawili wadogo ambao wanaonekana kumpenda sana.

•Mama huyo wa watoto watatu alionekana kuzidiwa na hisia alipokuwa akiwakumbatia watoto wa mwajiri wake.

amerejea Lebanon kwa mwajiri wake.
Nanny Rosie amerejea Lebanon kwa mwajiri wake.
Image: HISANI

Bi Roseline Atieno Oyola almaarufu Nanny Rosie, mwanamke Mkenya ambaye alivuma sana kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa mwaka jana kufuatia video yenye hisia kali ya yeye akiaga familia ya mwajiri wake wa Lebanon sasa amerejea katika nchi ya Mashariki ya Kati.

Rosie alitua Lebanon kwa muda usiojulikana na alikaribishwa kwenye uwanja wa ndege na mwajiri wake na watoto wake wawili wadogo ambao wanaonekana kumpenda sana.

Video iliyoshirikiwa na mwajiri wa Rosie inaonyesha watoto hao ambao amekuwa akihudumia wakimkimbilia kabla ya kuwakumbatia kwa upendo.

“Rosie umerudi. Umerudi hapa Rosie. Tuliku’miss,” mwajiri wa Rosie alisikika akisema kwa furaha kwenye video hiyo.

Mwanamke huyo Mkenya anayetoka Bondo katika Kaunti ya Siaya alionekana kuzidiwa na hisia alipokuwa akiwakumbatia watoto wa mwajiri wake.

"Niliwa’miss sana," Rosie aliwaambia watoto hao wawili kwa hisia nyingi.

Mama huyo wa watoto watatu amerejea Lebanon karibu miezi miwili baada ya kuiaga nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ili kuwa na familia yake iliyoko Kenya.

Hatua hii inajiri licha ya mwajiri wa Rosie kumshauri dhidi ya kurejea kazini Lebanon ili kubaki nchini Kenya na familia yake.

Mwezi uliopita, bosi wa Rosie, anayetambuliwa kama Maria Cataleya kwenye mtandao wa Tiktok alieleza kwamba alitumai Rosie angerudi lakini moyoni mwake anatumai hatarudi. Kwa nini? uliuliza.

Akjibu, "Kweli Maria ni mtu mwenye utu kabisa. Bila shaka, natumai atarudi. Lakini sidhani hivyo. Ni kama sitaki arudi. Nataka afurahie wakati wake na watoto wake na labda abaki nao,"

Mwajiri huyo wa Lebanon alisema katika video ya TikTok iliyokusanya zaidi ya watazamaji milioni 2.4 na kupendwa na zaidi ya 106.1k saa 24  tu baada ya kuchapishwa.

Mama huyo wa watoto 4 aliongeza; "Kama ningekuwa yeye, ningebaki Kenya na watoto wangu. Nisingerudi Lebanon, lakini ni juu yake."

Maria aliendelea kueleza waziwazi kuwa anahisi video ya kihisia iliyovuma kwenye mitandao ya kijamii ingeweza kufungua milango kwa fursa bora kwa Rosie nje ya Lebanon.

"Nina uhakika baada ya video hii ya mtandaoni, ataweza kupata fursa nyingine bora kuliko kurudi Lebanon," mwajiri wa Rosie alisema.