"Yatapumzika lini!" Mwanahabari wa 'Why are you gay?" alalamikia kufufuliwa kwa mahojiano hayo

"Mungu Mpendwa, Mahojiano haya yatapumzika lini?" Bw Simon Kaggwa alilalamika.

Muhtasari

•Mwanahabari Simon Kaggwa Njala amechoshwa na watu wanaoibua upya video ya mahojiano hayo yenye utata kila kukicha.

•Mahojiano hayo yamekuwa yakivunja mbavu za wengi kote ulimwenguni kutokana na jinsi Bw Kaggwa alivyoyaendesha wa njia ya ucheshi.

Image: TWITTER// SIMON KAGGWA NJALA

Mwanahabari wa Uganda aliyefanya mahojiano yaliyovuma ya ‘Why are you gay?’ zaidi ya muongo mmoja uliopita amechoshwa na watu wanaoibua upya video ya mahojiano hayo yenye utata kila kukicha.

Mwaka wa 2012, mwanahabari Simon Kaggwa Njala alimhoji mwanaharakati wa haki za wapenzi wa jinsia moja nchini Uganda,  Pepe Julian Onziema katika kipindi chake cha Morning Breeze kwenye steseheni ya CBS TV na tangu wakati huo mahojiano hayo yamekuwa yakivunja mbavu za wengi kote ulimwenguni kutokana na jinsi alivyoyaendesha wa njia ya ucheshi.

Hivi majuzi, mtumizi wa mitandao alitengeneza video ya katuni ya mahojiano hayo na kuichapishwa kwenye mtandao wa Twitter akimsifu mwanahabari huyo kwa jinsi alivyofanya mahojiano hayo.

"Forever goated @SimonKaggwaNjal," mtumiaji wa Twitter kwa jina @Abrahamlyon1 aliandika chini ya video hiyo.

Bw Kaggwa hata hivyo alionekana kutopenda wazo la mahojiano hayo kufufuliwa upya na akajibu, “Dear Lord, When will this interview rest?”

Kumaanisha: Mungu Mpendwa, Mahojiano haya yatapumzika lini?

Si mara ya kwanza kwa mwanahabari huyo wa Uganda kulalamika kuhusu mahojiano aliyofanya muongo mmoja uliopita kurejeshwa.

Mwaka jana, akaunti ya Twitter @AfricaFactsZone ilichapisha klipu fupi ya mahojiano hayo na kuyataja kama mahojiano maarufu zaidi nchini Uganda.

"Mahojiano maarufu zaidi nchini Uganda. Mwandishi wa habari anauliza mtu kuhusu jinsia yake," maelezo ya video hiyo yalisoma.

Kaggwa ambaye alionekana kuchoshwa na video hiyo kuzungumziwa mara kwa mara alijibu, "Lakini kusema kweli, hii ilikuwa miaka kumi iliyopita! Boy child  ameteseka. "

Jibu la mwanahabari huyo lilidokeza kwamba mahojiano hayo huenda yalimletea matatizo fulani yasiyojulikana.

Wakati wa mahojiano na Pepe Onziema mwongo mmoja uliopita, Bw Kaggwa alionekana kukerwa na sababu ya mwanaharakati huyo wa haki za binadamu kuchagua kuwa shoga na alitaka sana kuelewa yeye ni nani hasa.

"Why are you gay? (Kwa nini wewe ni shoga)?" Kaggwa aliuliza mara kwa mara huku mahojiano yakiendelea.

Onziema ambaye alizaliwa mwanamke hata hivyo hakutaka kuitwa shoga na kusisitiza kuwa yeye ni mwanamume anayevutiwa na wanamke.

"Mimi si mwanaharakati wa haki za binadamu anayetetea usawa kwa watu wenye mtazamo tofauti wa kimapenzi na ujinsia tofauti," alisema.

Onziema pia alikiri kuwa na mpenzi mwanamke lakini akaweka wazi kuwa hakuwa akishiriki tendo la ndoa naye.

Alipuuzilia mbali madai kwamba alikuwa akipigia debe ushoga nchini Uganda na akakana kuwa alilipwa kufanya hivyo.